Watu 75 wafariki kwa ajali ya treni DRC
Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya treni kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo sasa imefikia 75 , hii ni kwa mujibu wa maafisa wa Shirika la reli na Wizara ya Mawaasiliano.


Maafisa hao wanasema idadi ya majeruhi ni 125 wengi wao wakiwa ni akina mama na watoto.


Idadi hii mpya imetangazwa na Mkurugenzi wa shirika la Reli Bwana Abien Mutomb, baada ya kutembelea eneo la ajali hiyo akandamana na timu maalum iliyoundwa kuchunguza mkasa huo.


Siku ya Jumamosi maafisa wa shirika la reli walikuwa wamethibitisha kuwa idadi ya waliofariki ilikuwa watu 61 wakiwemo wanawake na watoto .Taarifa hiyo ya Jumamosi ilimnukuu Marc Manyonga Ndambo, Mkurugenzi wa miundo mbinu akizungumza na chombo cha Habari cha AFP kuwa watu 52 waliojeruhiwa waliokolewa.


Vyombo vya Habari nchini humo vilimnukuu gavana wa jimbo hilo Fifi Mazuka akisema kwamba takriban watu 60 wamefariki.

‘’Ilikuwa treni ya mizigo iliokuwa ikibeba mamia ya watu waliokuwa wakisafiri kutoka eneo moja hadi jingine kwa njia ya siri’’, alisema bwana Manyonga.


Baadhi ya miili ilikwama katika mabehewa ambayo yalikuwa yameanguka, aliongeza. Manyonga alisema kwamba treni hiyo ilikuwa na mabehewa 15, 12 kati yake yalikuwa hayana mzigo.


Treni hiyo ilikuwa inatoka Luen kuelekea katika mji wa migodi wa Tenke, karibu na Kolwezi mji mkuu wa Lualaba kusini mwa DRC.

Ilikosa mwelekeo siku ya Alhamisi karibu na Kijiji cha Buyofwe takriban kilomita 200 kutoka Kolwezi katika eneo lenye mabonde ambapo mabehewa 7 yalianguka, alisema.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu