Watu 46 wakutwa wamefariki kwenye lori lililotelekezwa MarekaniTakriban watu 46, wanaoaminika kuwa wahamiaji, wamepatikana wamefariki kwenye lori lililotelekezwa katika eneo la San Antonio, Texas Marekani.


Charles Hood, Mkuu wa Zimamoto wa eneo la San Antonio kulipotokea mkasa huo alisema mbali na vifo vya watu hao pia manusura 16 wakiwemo watoto wanne wamepelekwa hospitalini kwa matibabu .


Walionusurika walikuwa moto ‘’kugusika‘’ na wanakabiliwa na kiharusi cha joto na uchovu wa joto.

San Antonio, ambayo ni 250km (maili 150) kutoka mpaka wa Marekani na Mexico, ni njia kuu ya kupita kwa watu wanaosafirishwa kwa njia haramu.


Aliongeza kuwa lori hilo halikuwa na kiyoyozi kinachofanya kazi na kwamba ndani yake hakukuwa na maji.


Kwa mujibu wa kituo cha runinga cha KSAT, gari hilo liligunduliwa karibu na njia za reli katika Upande wa Kusini Magharibi mwa San Antonio.


Idadi kubwa ya wahudumu wa dharura, wakiwemo polisi, wazima moto na wahudumu wa gari la wagonjwa, walionekana wakizunguka lori hilo kubwa.


Mkuu wa Polisi wa San Antonio William McManus alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ingawa sasa umekabidhiwa kwa serikali kuu na watu watatu wamekamatwa.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico, Marcelo Ebrard, alisema balozi mdogo wa nchi hiyo alikuwa njiani kuelekea eneo la tukio, lakini akaongeza kuwa mataifa ya waathiriwa bado hayajajulikana.


Gavana wa chama cha Republican cha Texas Greg Abbott alimlaumu Rais wa Marekani Joe Biden kwa vifo hivyo, akivitaja kama ‘’matokeo ya sera zake mbaya za mpakani’’.


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu