Wataalamu wahimiza kupima homa ya iniWataalamu wa afya wamesema kuna umuhimu wa kupima damu kujua hali ya maambukizo ya homa ya ini ili kujitibu mapema, kwa kuwa dalili za ugonjwa huo huanza kuonekana baada ya miaka 15 hadi 20.


Wanasema huenda maambukizo ya homa hiyo ni zaidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).


Pia, kati ya watu 100, wanane wanaweza kuwa na maambukizo sugu ya ugonjwa huo na wasionyeshe dalili.


Wakati haya yakisemwa, tayari watu waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2017 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ulionyesha maambukizi ni asilimia 4.0 kwa Watanzania wenye umri kati ya miaka 15-49.


Takwimu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), zinaonyesha maambukizo ya homa ya ini B miongoni mwa wachangiaji damu kwa mwaka 2021 ni asilimia 5.3.


Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na ini kutoka Hospitali ya Aga Khan, Maswola Ng’wanasayi amesema juzi kuwa japokuwa bado takwimu mpya hazijatolewa za hali ya maambukizo nchini, umakini na uhakiki wa kujua hali ya afya ni muhimu ili kuepuka madhara ya baadaye.


“Kwa sasa wengi wanaobainika wale wanaochangia damu, utafiti wa mwisho ulikuwa mwaka 2019 ulionyesha asilimia 4 wenye maambukizi wakati wenye virusi vya Ukimwi ni asilimia 5, lakini utofauti hapo wengi wenye homa sugu ya ini ni vigumu kubaini kwa kuwa hawapimi na huathiri baadaye sana,” alisema Dk Ng’wanasayi.


“Walio na maambukizo ya VVU wengi wanajua na wanatumia dawa, lakini wenye maambukizi ya homa ya ini anaweza akawa anapima tu VVU anajikuta mzima kumbe ana homa ya ini hawa hawana taarifa sababu hawajawahi kupima. Asipopima na ugonjwa hauonyeshi dalili hatajua mpaka ini litakapokuwa limeharibika miaka 15 mpaka 20,” alisema Dk Ng’wanasayi.


Alisema iwapo mtu atabaini mapema itakuwa ni rahisi kupata matibabu na ataweza kuzuia saratani ya ini.


Dk Ng’wanasayi alisema ugonjwa huo ni hatari zaidi kwa kuwa unaambukiza kupitia njia zote ambazo husababisha maambukizi ya VVU kama kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana, utumiaji usio salama wa sindano na kujichoma na vitu vyenye ncha kali.


Pia, majimaji ya mgonjwa kumpata mtu mwingine kama ana kidonda, mama anaweza kumwambukiza mtoto wake wakati wa kujifungua.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu