Wananchi wamtoa mtuhumiwa Polisi, wamuua MorogoroMwanaume aliyetambuliwa kwa jina la Ally Ally aliyekuwa akituhumiwa kumuua mwenzake aliyefahamika kwa jina la Kibwana Musa (32) mkazi wa Kijiji cha Kiziwa A, kata ya Kiroka Morogoro kwa madai ya kumfumania na mwanamke wake, naye ameuawa kwa kupigwa na mawe na kukatwa katwa na mapanga na wananchi wenye hasira kali muda mfupi baada ya kumkamata.


Akizungumzia tukio hilo Jumatano, Juni 29, 2022, diwani wa Kata ya Tegetelo alikokamatiwa Ally, Yusuph Gomba alisema alikamatwa Juni 27 Saa 10 alasiri ikiwa ni wiki moja imepita tangu alipofanya mauaji hayo.


“Baada ya kufanya tukio hilo, tulimkamata na kumuhifadhi Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Tegetelo kwa ajili ya usalama wake na tulipiga simu polisi kwa ajili ya kuomba msaada wa askari na usafiri wa kumfikisha kituo cha polisi Mkuyuni.


"Wakati tukisubiri askari polisi waje na usafiri, makundi makubwa ya watu waliokuwa na silaha za kila aina walikuwa nje ya ofisi ya mtendaji na muda wote walikuwa wakitaka tumtoe nje yule kijana ili wamuue kama alivyomuua mwenzake. Mimi na viongozi wenzangu tulijitahidi kuwasihi wananchi na nashukuru walinisikiliza," alisema Gonna.


Alisema kuwa majira ya saa 4 usiku askari polisi wawili mmoja akiwa na silaha (bunduki) walifika katika ofisi ya mtendaji Kata ya Tegetelo kwa ajili ya kumchukua Ally ambaye muda wote alikuwa chini ya ulinzi wa viongozi wa kata, kijiji na askari wa jeshi la akiba (mgambo) na baada ya kukabidhiwa polisi waliondoka Ally kwa kutumia usafiri wa pikipiki.


"Walitumia pikipiki moja ambapo askari mmoja alikuwa ndio akiendesha pikipiki hiyo na askari mwingine alikaa nyuma ya mtuhumiwa, hata hivyo baada ya kuondoka makundi makubwa ya wananchi waliokuwa na bodaboda walianza kuwafuatilia askari hao, kiukweli ilikuwa hatari kwa sababu wananchi wale walikuwa na hasira na walikuwa na silaha, maana kabla polisi hawajafika walitaka kuchoma moto ofisi ya kata tulikomhifadhi yule mtuhumiwa," alisema Gonna.


Aliongeza kuwa pamoja na askari polisi lakini pia ndugu wa marehemu Kibwana nao walikuwa na pikipiki ambapo waliongozana na askari hao.

Alisema kuwa wakiwa njiani kuelekea Kituo cha Polisi Mkuyuni walipofika eneo la Shule ya Msingi Magawe, Kata ya Kinole kundi la wananchi lilifunga barabara kisha kuweka mawe na magogo.

Hivyo kusababisha pikipiki waliyopanda askari na mtuhumiwa ilianguka ambapo askari hao walipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili na hivyo wananchi hao waliokuwa na mapanga, shoka na silaha mbalimbali walimteka mtuhumiwa na kukimbia naye kitongoji cha jirani na kuanza kumpiga mawe na kumkatakata kwa mapanga hadi kufariki dunia.

Diwani huyo alisema kuwa awali kabla mtuhumiwa huyo kuondolewa ofisi ya kata, inaelezwa kwamba alikiri kumuua Kibwana kwa kile alichodai kuwa alikuwa akitembea na mwanamke wake aliyetajwa kwa jina la Farida Ally.

Hata hivyo aliomba kama naye atauawa basi mwili wake ukazikwe kwa babu yake Kijiji cha Kungwe kilichopo Kata ya Tomondo.

Katika hatua nyingine diwani huyo aliiomba Serikali kujenga vituo vya polisi vya kata ili kusogeza huduma ya kiusalama kwa wananchi na watuhumiwa hasa yanapotokea matukio ya uhalifu.


"Yule mtuhumiwa aliuawa kwa sababu Kata Tegetelo haina kituo cha polisi. Hata hivyo, wananchi walituzidi nguvu na pia usafiri waliotumia askari waliokuja kumfuata mtuhumiwa haukuwa wa usalama, kama wangekuja na gari na askari wa kutosha wenye silaha na mabomu ya machozi wale wananchi wangehofia kufanya waliyoyafanya," alisema Gonna.


Awali, akizungumzia mazingira waliyomkamatia mtuhumiwa huyo kabla ya kuuawa Gomba alisema kuwa yeye na viongozi wenzake walipata taarifa ya kuwepo kwa mtu ambaye hafahamiki katika kata hiyo ambaye alikuwa amefikia kwa babu mmoja ambaye alikuwa akiishi na mke wake na baada ya kufuatialia waligundua kuwa mtu huyo alikuwa mgeni katika eneo hilo ambapo mke wa babu huyo ndio alikuwa bibi wa mtuhumiwa ambaye kwa sasa ni marehemu.


Alisema kufuatia taarifa hizo uongozi wa kata na Kijiji ulimtilia mashaka na kuanza kufuatialia nyendo zake ambapo waligundua kuwa mtu huyo nyakati za mchaa alikuwa akijifungia ndani na ibapofika jioni ndio alikuwa akitoka nje.


Gomba alisema kuwa kutokana na hali hiyo walitoa taarifa kwa vijiji vya jirani kikiwemo Kijiji alichofanya mauaji na baada ya kueleza namna alivyo ndugu wa marehemu kibwana waliamua kwenda kuweka mtego na waliweza kumtambua kuwa ndio mtu aliyehusika na mauaji ya ndugu yao.

"Hapo Sasa ndio tukaanza kuweka mitego na ilipofika Juni 27 majira ya saa 10 mtuhumiwa huyo alitoka nje kuwapokea mzigo bibi na babu yake na hapo ndio tunamsubiri aingie ndani na kumkamata, baada ya kumkamata yule bibi na babu yake hawakufahamu kama mjukuu wao alifanya mauaji na kukimbilia kwao hivyo tuliwaacha pale nyumbani na sisi tuliamua kumchukua mtuhumiwa na kumpeleka ofisi ya kata ya Tegetelo kwa ajili ya kusubiri polisi," alisema Gomba.

Kwa upande wake kaka wa marehemu Kibwana, Juma Musa alisema kuwa baada ya mdogo wake kuuawa walianza kazi ya kumsaka muhusika wa mauaji hayo ambapo walisambaza picha vijiji vingi vya jirani na ilipofika Juni 27 walipata taarifa ya kuonekana kwa mtuhumiwa huyo kata ya Tegetelo.


Juma alisema kuwa akiwa na ndugu zake wengine pamoja na marafiki wa marehemu walikwenda Tegetelo na kuweka mitego ambapo waliweza kumuona mtuhumiwa huyo hivyo waliwasiliana na uongozi na kufanikiwa kumkamata.


"Baada ya muda mfupi taarifa zilisambaa vijiji vingi na tukiwa na mtuhumiwa tulipata taarifa kuwa makundi ya watu wamejificha porini kwa nia ya kumteka mtuhumiwa ili naye wamuue, kwa vile Mimi lengo langu afike Salama polisi nilijitahidi kuwasihi baadhi ya vijana wenzangu wasifanye hivyo lakini waliniambia kama wakimkosa mtuhumiwa basi wataniua mimi, kiukweli polisi kilichotokea ni kwamba polisi walikuwa wachache na walizidiwa nguvu kwa wingi wa watu wale, silaha walizokuwa nazo ilibidi waje askari wa kutosha wenye silaha za moto," alisema Juma.


Alisema kuwa pamoja na kumuua lakini pia wananchi hao walichoma moto nyumba ya Ally na kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa ndani ya nyumba hiyo.


Kufuatia tukio hilo la mauaji ya kisasi kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Fotunatus Musilimu alisema kuwa askari walipata majeraha baada ya pikipiki waliyokuwa wamepanda na mtuhumiwa kuangua kufuatia magogo na mawe yaliyotegeshwa na wananchi barabarani.


Hata hivyo alisema kuwa kitendo walichofanya wananchi ni kosa kwa kuwa wamejichukulia sheria mikononi na pia kungeweza kuhatarisha usalama wa raia wengine endapo askari angetumia nguvu kubwa na kwamba uchunguzi wa matukio yote unaendelea kufanywa.


Farida ambaye alikuwa chanzo cha mauaji hayo kwa sasa anaendelea na matibabu kwa kuwa naye alijeruhiwa kwa kukatwa panga mkononi na baada ya marehemu Ally kumkuta nyumbani kwake akiwa na Kibwana ambaye naye ni marehemu.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu