Waafrika zaidi ya elfu 3 wafariki wakijaribu kuvuka bahari kutafuta maisha Ulaya mwaka jana pekeeHii ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR inayohusu kipindi cha mwaka jana pekee.


Kwa mujibu wa shirika hilo mwaka jana 2021, watu 1,924 waliripotiwa kufariki dunia au kupotea wakiwa safarini kupitia bahari ya Mediterania, huku wengine 1,153 wakipoteza maisha au kupotea kwenye njia ya kupitia baharini ya Kaskazini Magharibi mwa Afrika kuelekea visiwa vya Canary.


Idadi ya vifo vilivyoripotiwa mwaka 2020 ilikuwa 1,544 kwa njia hizo mbili na UNHCR inasema inatia hofu kwamba, tangu mwanzo wa mwaka huu, watu wengine 478 pia wamekufa au kupotea baharini.


Shirika hilo la wakimbizi limesema safari nyingi za vivuko vya baharini zilifanyika katika boti zilizojaa kupitiliza, zisizostahili kwa safari hizo za majini, na zenye kujazwa hewa na nyingi kati ya hizo zilipinduka au kuharibika na kusababisha kupoteza Maisha ya watu wengi.


Safari za baharini kutoka mataifa ya pwani ya Afrika Magharibi kama vile Senegal na Mauritania hadi visiwa vya Canary ni ndefu na za hatari na zinaweza kuchukua hadi siku 10 kuwasili limesema shirika hilo la wakimbizi.


Limeongeza kuwa boti nyingi zilizama au kupotea bila kujulikana zilipo katika maji hayo.


UNHCR inasema njia za nchi kavu pia zinaendelea kuwa hatari sana, ambapo huenda idadi kubwa zaidi ya watu walikufa katika safari kupitia Jangwa la Sahara na maeneo ya mpakani ya mbali, katika vituo vya kizuizini, au walipokuwa katika utumwa wa wasafirishaji haramu.


Miongoni mwa orodha ya dhuluma zinazoripotiwa na watu wanaosafiri katika njia hizi ni pamoja na mauaji ya kiholela, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria na kiholela, unyanyasaji wa kingono na kijinsia, kazi za kushurutishwa, utumwa, ndoa za kulazimishwa na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu