Sasa ni lazima kuvaa barakoa katika maeneo ya umma KenyaWaziri wa Afya nchini Kenya, Mutahi Kagwe ametangaza kurejea kwa uvaaji wa barakoa wa lazima katika maeneo ya usafiri wa umma, ndege, ofisini katika maduka makubwa na maeneo ya ibada.


Kufuata taarifa zinazotolewa na wizara hiyo mara kwa mara kufahamisha watu jinsi hali inavyoedelea, waziri alieleza kwamba maambukizi yamekuwa yakiongezeka katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

‘’Ongezeko la taratibu limeshuhudiwa kutoka asilimia 0.6 mwanzoni mwa mwezi mei 2022 hadi wastani wa kila wiki wa asilimia 10.74 katika wiki iliyoisha ya Juni 19 2022,’’ Waziri kangwe alisema.


Ameongeza kuwa kwa kasi hii ya ongezeko la maambukizi ni wakati raia wanastahili kuchukua hatua ili kuepuka kilichoshuhudiwa mwaka 2020 na 2021 kupoteza maisha ya watu wengi na mali.


Mikutano ya pamoja ya watu wengi katika sehemu moja ya ndani, imeruhusiwa mradi washiriki wote wawe wamepata chanjo. Lakini pia imekuwa lazima kwa wote kuvaa barakoa na pia waonyeshe thibitisho kwamba wamepata chanjo.


Hali ilikuwa hiyo hiyo kwa maeneo ya kuabudu.


‘’Idadi ya watu katika maeneo ya kuabudu haina kikomo mradi wote waliokusanyika wamepata chanjo kikamilifu. Pia wote watatakiwa kuvaa barakoa wakiwa ndani ya maeneo ya kuabudu.’’


Wakati huo huo, Bwana Kagwe aliomba wale ambao bado hawajapokea chanjo, kuchanjwa kwa haraka sana akisema Wakenya wote wanapaswa kuchukua tahadhari.


‘’Wale ambao hawajachanjwa wafanye hivyo mara moja. Waliochanjwa na wanaohitaji nyongeza, pia wafanye hivyo mara moja,’’ Kagwe alisema.


Kagwe aliongeza kuwa hali ya maambukizi huenda ikawa mbaya zaidi katika wiki zijazo kutokana na msimu huu ambao ni hali ya hewa ya baridi.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu