Rwanda yakanusha madai ya kuunga mkono waasi wa M23 walioanzisha vita DRCRwanda imekanusha kuwa jeshi lake, linaunga mkono waasi wa M23 waliopambana na wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Jumatatu.


Madai hayo yamekanushwa na Gavana wa Rwanda wa mkoa wa Magharibi Francois Habitegeko ambaye katika taarifa yake, amesema madai hayo yanalenga kuliharibia jina nchi yake.


Aidha, amesema watu wawili aliosema wanaaminiwa kuwa wanajeshi wa Rwanda, walikamatwa mwezi mmoja uliopita na kinachoendelea ni upotoshaji.


Hii inakuja baada ya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kuishtumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao, kutekeleza mashambulizi katika ardhi yake.


Siku ya Jumatatu, waasi hao wa M23 walitekeleza mashambulizi katika vijiji vya Tchanzu na Runyoni wilayani Rutshuru kwa mujibu wa kiongozi wa kijeshi katika eneo hilo, Sylvain Ekenge.


Ripoti kutoka kwa mashirika ya kiraia Mashariki mwa nchi hiyo, zinasema mapigano yamerejelewa tena kati ya waasi hao na wanajeshi wa serikali.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu