Rais wa Marekani akataa kuomba radhi kwa kauli ya kutaka Putin aondolewe madarakaniRais wa Marekani, Joe Biden amesema hatoomba radhi kutokana na kauli yake aliyoitoa kwamba Rais wa Urusi Vladmir Putin hawezi kuendelea kubakia madarakani, akifafanua kuwa matamshi hayo yalionesha ''ghadhabu yake ya kimaadili'' na sio ''mabadiliko ya sera'' .


Akizungumza na waandishi habari katika Ikulu ya Marekani, Biden amesema anataka kuweka wazi kwamba hatoi wito wa kuwepo mabadiliko ya sera nchini Urusi na hivyo hatoomba msamaha kutokana na kuelezea hisia zake binafsi.


Biden amesema hana wasiwasi kwamba matamshi yake aliyoyatoa wakati akiwa ziarani mjini Warsaw, Poland, yatazidisha mvutano kuhusu vita vya Ukraine.


Rais huyo wa Marekani amesema alikuwa akielezea hisia zake kuhusu Putin na kwamba tabia yake haikubaliki kabisa na sio kutaka mabadiliko.


Biden amesema jambo la mwisho analotaka kuliona ni kujihusisha na vita vya ardhini au vita vya nyuklia na Urusi.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu