Ofisi ya Msajili yabariki kusimamishwa kina MbatiaOfisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imemsimamisha Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia na Sekretarieti yake yote, kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapoamuliwa vinginevyo.


Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Mei 25, 2022 na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza akisema uamuzi wa Kikao cha Halmashauria ya chama hicho kilichofanyika Mei 21 mwaka huu, ulikuwa halali kwa akidi ya wajumbe wake licha ya kutotaja uhalali wa akidi hiyo.


Nyahoza amesema kwa mamlaka ya ofisi hiyo, inamtaka Mbatia kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapotenguliwa na chama.


“Baada ya kusimamishwa, katibu wa chama hicho alituletea barua kwa fomu ya kisheria inayotujulisha kusimamishwa uanachama, tumekubaliana na uamuzi huo. Kama hawataridhika (Kina Mbatia) ziko njia za kutafuta haki, waende mahakamani,”amesema Nyahoza.


Jumamosi Mei 21 mwaka huu, Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi ilimsimamisha Mbatia na makamu Mwenyekiti Bara, Angelina Mtahiwa kutojihusisha na shughuli zozote za chama hadi mkutano mkuu utakapoitishwa ili wajieleze kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.


Mbatia na wenzake walisimamishwa kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwamo kugombanisha viongozi na hivyo kulazimisha kujiuzulu.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu