Mwenye ulemavu wa macho atunukiwa PhD UDSMMwalimu Celestine Karuhawe ameyafanya Mahafali ya 52 ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa ya kipekee baada ya kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Elimu (PhD) akiwa ni mhitimu pekee kati ya 68 ambaye ni mlemavu wa macho.


Dk Karuhawe alitunukiwa Shahada ya Falsafa katika Elimu kwenye mahafali ya hayo yalifanyika Alhamisi Juni 2, 2022 jijini Dar es Salaam.


Daktari huyo mpya ni miongoni mwa wahitimu 68 wa PhD ambao kati yao 36 walikuwa wanawake.


Baada ya kutunukiwa, Dk Karuhawe alisema mafanikio yake ni uthibitisho wa dhamira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kutoa elimu kwa wote, wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum kama yeye.


"Dhana kwamba mazingira ya kujifunzia yasiwe kikwazo kwa wengine hasa wenye ulemavu kupata elimu wanayoitaka, ni ukweli uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimejitahidi katika hilo," alisema Dk Karuhawe.


Dk Karuhawe ambaye ana taaluma ya ualimu na mwenye uzoefu wa kufundisha katika shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu nchini alitoa rai kwa chuo hicho kuendelea kutoa ushirikiano na kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa wote, hasa kwa kuwekeza kwenye vifaa vya kisasa vya kujifunzia vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa wale wenye mahitaji maalumu, pamoja na kujenga miundombinu muhimu.


Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha UDSM (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa, alimpongeza Dk Kipengele kwa mafanikio hayo akisema kuwa kuhitimu kwa mwalimu huyo kumeyafanya mahafali ya 52 kuwa ya kipakee.


Naye Mkurugenzi wa Mafunzo ya Uzamili, Profesa Donatha Tibuhwa alisema mafanikio ya Dk Karuhawe yanapaswa kuwa hamasa na kutoa wito kwa wengine kujiunga na masomo UDSM kwa kuwa kuna vifaa na wahadhiri wa kutosha kuwasaidia wanafunzi kumaliza masomo yao kwa ufanisi.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu