Mwanafunzi uandishi wa habari UDSM auawa na kundi la Panya roadMwanafunzi wa stashahada ya uandishi wa habari mwaka wa pili katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Maria Basso (24) amefariki dunia baada ya watu zaidi ya 10 kuvamia nyumbani kwao Kawe Mzimuni.


Taarifa iliyotolewa Jumatano Septemba 14,2022 na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Wiliam Mkonda imedhibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo Septemba 14 saa 2:30 usiku maeneo ya Kawe mzimuni, kikundi cha wahalifu wakiwa na silaha za jadi, walivamia nyumbani kwa jina Paschal Basso (56).


Amesema baada ya kuvamia nyumba hiyo yenye vyumba 15, walivunja milango na kupora fedha, simu za mkononi, kujeruhi watu watatu na kumuua mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Maria Paschal (24).


"Tukio walilofanya wahalifu hawa ni baya na linalotakiwa kulaaniwa na kukemewa na Mtanzania yoyote anayechukia uhalifu kwa watu kama hawa ambao hawataki kutumia njia halali za kujitafutia kipato," amesema Kamanda Mkonda.


Kufuatia tukio hili, Jeshi la Polisi Kanda Maalum linawasaka wahalifu wote waliohusika katika tukio hilo pamoja na kuimarisha doria za miguu na magari katika maeneo yote.


“Tunaendelea kuwasisitiza viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika kukabiliana na uhalifu wa aina hii katika maeneo yao,” amesema.Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu