Mamilioni ya vijana na hatari ya kupoteza uwezo wa kusikiaJe wafahamu zaidi ya watu bilioni 1 wenye umri wa kuanzia miaka 12 hadi 35 wako hatarini kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia kutokana na masikio hayo kupata sauti kubwa kupita kiasi iwe kwa mtu kusikiliza mwenyewe au sauti zitokazo katika vipaza sauti vya shughuli za kijamii au umma?


Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema kuwa iwapo mwelekeo wa sasa wa kusikiliza kitu masikioni kwa sauti kubwa utaendelea, basi kuna madhara makubwa kwa afya ya mwili na akili.


Mkurugenzi wa Idara ya WHO ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dkt. Bente Mikkelsen amesema mamilioni ya watoto na vijana wako hatarini kupoteza uwezo wao wa kusikia kutokana na matumizi yasiyo salama ya vifaa vya kusikilizia sauti masikioni sambamba na sauti kubwa kwenye kumbi za vilabu vya usiku, matamasha na michezo.


Amesema hatari inaongezeka zaidi kwa kuwa vifaa vingi vya kusikilizia sauti, kumbi na matukio ya umma hayana maonyo au viwango vya usikilizaji na hivyo kusababisha hatari ya kupoteza usikivu kwa kuwa sauti huwa kubwa kupindukia.


WHO imeweka mapendekezo sita ya viwango vipya vya sauti ya kusikiliza katika kumbi za starehe na michezo ili kulinda watoto na vijana dhidi ya kupoteza uwezo wa kusikia.


1. Wastani wa kiwango cha juu kisizidi 100 katika kipimo cha sauti. 2. Kuwepo kwa mfanyakazi anayefuatilia kiwango cha sauti kisizidi kiwango hicho cha 100. 3. Kuwepo kwa vifaa vya kudhibiti sauti kuenea maeneo mengine nje ya eneo husika ili usikivu usiwe wa vurugu. 4. Kuhakikisha kuna vifaa vya mtu kuweza kusikiliza binafsi na kuweko na maelezo ya matumizi. 5. Kuweko na eneo tulivu kwa watu wasiopenda kelele ili kupunguza hatari ya kupoteza usikivu 6. Wafanyakazi kupatiwa mafunzo na taarifa kuhusu umuhimu wa kulinda usikivu bora


Ukipoteza uwezo wa kusikia hakuna tiba, bali kuna kinga

WHO inasema kuwa kupoteza uwezo wa kusikia ni tatizo ambazo haliwezi kupatiwa tiba lakini linaweza kuzuilika. Ni kwa mantiki hiyo shirika hilo linataka vijana kuchukua hatua kwa kuhakikisha sauti inakuwa ya chini pindi wanapotumia vifaa vya kusikilizia masikioni. Halikadhalika vifaa hivyo viwe ni vile vinavyokata sauti za nje, kuvaa vizuia sauti kwenye kumbi zenye kelele kubwa na kufanya mara kwa mara uchunguzi wa uwezo wa sikio kusikia.


WHO inasihi serikali kuandaa sheria za usikikilizaji ulio salama na kuelimisha jamii kuhusu changamozo za kupoteza usikivu. Sekta binafsi nazo zinapaswa kujumuisha mapendekezo ya WHO kwenye bidhaa zao, kumbi na matukio. Na ili kuchagiza usikilizaji usio hatarini, WHO inataka uhamasishaji wa ubadilishaji tabia ufanywe na mashirika ya kiraia, wazazi, walimu, madaktari na kadhalika.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu