Mahakama yafuta hukumu ya aliyepelekwa gerezani kwa uchawiMahakama Kuu imetengua kifungo cha miaka mitano jela dhidi ya mkazi wa Kijiji cha Lwela, Mkoani Njombe, John Severine Chale (60) alichohukumiwa kwa madai ya kumloga na kumsababishia ukichaa mtoto wa mdogo wake.


Hukumu dhidi ya Chale ilitolewa na Mahakama ya Wilaya ya Ludewa Agosti 29 mwaka huu baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka.


Kufuatia hukumu hiyo, Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ililazimika kuita jalada la kesi hiyo ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wa hukumu hiyo iliyotolewa na hakimu, Isaac Ayengo.


Mahakama Kuu ina haki ya kisheria kuitisha jalada la kesi yoyote iliyoamuliwa na mahakama za chini ili kujiridhisha kama ilizingatia sheria.


Akisoma hukumu iliyotengua kifungo hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, John Utamwa alisema baada ya kupitia vifungu vya sheria, mahakama hiyo ilijiridhisha kuwa kifungu cha (3) cha Sheria ya Uchawi kilichotumika kumtia mtuhumiwa hatiani hakikuhusika.


Kifungu hicho kinatamka kuwa mtu yeyote ambaye kwa matamshi au matendo yake hujionesha kuwa na nguvu za kichawi, au anamiliki vifaa vinavyoaminika kutumika kwa uchawi, au anasambaza vifaa hivyo, au anatoa ushauri kuhusu uchawi au kutishia kutumia uchawi dhidi ya mtu yeyote au vitu, atakuwa ametenda kosa la jinai.


Alisema katika hukumu iliyosomwa kwa njia ya mtandao kuwa mahakama hiyo imekubaliana na Wakili wa Serikali, Basilius Namkambe, aliyetaka mahakama kubatilisha huku hiyo.


Ameongeza kuwa John alishitakiwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Uchawi kinachozungumzia uchawi lakini maelezo ya kosa yaliyowasilishwa mahakamani yalimtaja mshtakiwa kujihusisha na vitendo vya kishirikina, hivyo kushindwa kutofautisha ushirikina na uchawi.


Kifungu cha 5 cha Sheria ya Uchawi kinatamka kuwa mtu yeyote anayetenda kosa la uchawi kwa lengo la kusababisha kifo, ugonjwa, majeraha au madhila kwa jamii yoyote, mtu au wanyama atastahili kifungo kisichopungua miaka saba.


Jaji Utamwa amesema kutokana na makosa hayo ya kisheria, mahakama imebatilisha mwenendo wa shauri hilo na kutengua adhabu aliyopewa Chale kwa kwenda kinyume na kifungu cha 5 (1) (a) cha Sheria ya Uchawi.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu