Kifo cha rais Haiti bado kizungumkutiHaiti jana Alhamisi iliadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu rais Jovenel Moise alipouawa kwa kupigwa risasi katika makaazi yake ya kibinafsi, bila ya mhusika wa shambulio hilo kutambuliwa na uchunguzi juu ya mauaji hayo ukikwama.


Moise aliuawa mnamo Julai 7 mwaka jana, baada ya kundi la makomando kuingia nyumbani mwake huko Port-au-Prince na kumpiga risasi 12.


Polisi ya Haiti iliwakamata haraka takriban washukiwa 20, wakiwemo wanajeshi 18 wa zamani wa Colombia walioshukiwa kuajiriwa kama mamluki. Lakini tangu wakati huo, kumekuwa na maendeleo madogo katika uchunguzi wa mauaji hayo nchini Haiti na pia Marekani.


Waziri Mkuu Ariel Henry, ambaye alichukua wadhifa huo siku mbili tu kabla ya kifo cha Moise, anashukiwa kufanya mazungumzo na mmoja wa washukiwa wakuu wa mauaji ya Moise kwa njia ya simu punde tu baada ya shambulio hilo- japo amepuuza madai ya kuhusika na kifo hicho.


Bwana Henry alitoa hotuba jana Alhamisi katika halfa ndogo iliyosusiwa na mjane wa rais huyo, Martine Moise, ambaye alinusurika kifo japo alijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo.


Marekani imeitolea mwito Haiti kuongeza kasi ya uchunguzi wa mauaji hayo.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu