Kesi ya Mfalme Zumaridi yashindwa kuamuliwa baada ya hakimu kuuguaMahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza imeshindwa kutoa uamuzi mdogo wa maombi ya upande wa utetezi yaliyomtaka hakimu anayesikiliza kesi hiyo ya jinai namba 10/2022, Monica Ndyekobora kujiondoa kusikiliza kesi hiyo kwa kile ulichodai hauna imani na hakimu huyo.


Julai 11 mwaka huu, mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo yenye mashtaka matatu ikiwemo kushambulia na kuzuia maofisa wa umma kutekeleza majukumu yao, Diana Bundala maarufu kama "Mfalme Zumaridi" kupitia kwa wakili wake, Steven Kitale akisaidiana na Erick Mutta aliiambia mahakama hiyo kwamba hana imani na hakimu anayesikiliza kesi hiyo huku akimtaka kujiondoa.


Akizungumza leo Julai 18, 2022 ndani ya chumba cha mahakama hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga ameiambia mahakama hiyo kwamba kesi hiyo imeitwa leo kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo kuhusu maombi yaliyowasilishwa na mshtakiwa namba moja kwa hakimu huyo.


Kutokana na maombi hayo kuwasilishwa ofisini kwake, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Monica Ndyekobora aliahidi kutoa uamuzi mdogo wa maombi hayo leo Julai 18, 2022 jambo ambalo halikufajikiwa kwa kile alichodai kwamba alikuwa anaumwa hivyo hakupata wakati wa kutafakari kuhusu suala hilo.


"Maamuzi hayajakamilika kwa sababu nilikuwa naumwa kwa kipindi chote hadi leo, hivyo naahirisha kesi hii hadi Julai 27, 2022 Saa 4:20 asubuhi," amesema Ndyekobora


Katika hatua nyingine, Mahakama hiyo pia imeahirisha kesi ya jinai namba 11/2022 inayomkabili Mfalme Zumaridi peke yake hadi Agosti mosi mwaka huu Saa 4 asubuhi kwa kile kilichoelezwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga kwamba upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu