Kenya yapeleka madaktari wake hospitali za UingerezaWaziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe jana Jumatatu aliwaaga rasmi kundi la wauguzi 19 wa Kenya ambao wameajiriwa kufanya kazi nchini Uingereza.


Hii inafuatia makubaliano ya pande mbili kati ya Kenya na Uingereza yaliyotiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson Julai mwaka jana.


Bw Kagwe alisema kuwa mchakato mkali ulifanywa ili kupata orodha ya mwisho kutoka kwa wauguzi 3,329 waliotuma maombi mwaka jana.Kati ya 19 waliohitimu, 13 wataambatanishwa na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Oxford na wataondoka nchini Juni 28. Sita waliosalia ambao mahali pa kazi bado hapajatambuliwa, watasafiri hadi Uingereza baada ya wiki mbili.


Pia, wengine ni wauguzi 80 waliohitimu ambao watakuwa sehemu ya kundi la pili.


Bw Kagwe aliwataka wauguzi wengine pia kuangalia fursa kama hizo na kutuma maombi.


“Wahudumu wa afya wa Kenya wanapaswa kuwa na mawazo mapana. Ukweli kwamba ulifunzwa nchini Kenya hakupaswi kukuweka Kenya pekee. Fikiri kwa mapana na utafute fursa nje ya nchi. Hufanyi mazoezi ya maisha. Katika nafasi moja uliyonayo, panua fikra zako na ufanye kazi katika maeneo mengine,” alisema.


Alirejelea hitaji la Kenya kuwa kitovu cha utalii wa afya akisema kuwa kuajiri wauguzi hao hadi Uingereza kunaonyesha ubora wa mafunzo yaliyotolewa na taasisi zetu za ndani.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu