Hukumu ya rufaa ya Sabaya ni Mei 6 mwaka huuMahakama Kuu Kanda ya Arusha imepanga Mei 6, 2022 kutoa hukumu ya rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili wanaopinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Leo Machi 15, 2021 rufaa hiyo ya jinai namba 129/2021 ilipangwa kwa ajili ya kutajwa ambapo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Ruth Massam amesema hukumu hiyo itatolewa Mei 6, 2022.

Mbali na Sabaya waomba rufaa wengine ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura ambapo rufaa hiyo ilikuwa inasikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Sedekia Kisanya.

"Tumefikia mwisho wa usikilizwaji wa shauri na kama ambavyo awali niliwaeleza hili shauri lilipangwa kusikilizwa kwa mfumo wa session na muda ambao ulipangwa umemalizika. Shauri litakuja kwa ajili ya mention (kutajwa) Machi 15 na itapangwa uamuzi unatolewa lini," alisema Jaji Kisanya Februari 21, 2022 wakati wa kuhitimisha usikilizaji wa rufaa hiyo.

Rufaa hiyo iliyoanza kusikilizwa mfululizo Februari 15 mwaka huu inatokana na shauri la awali la jinai lililokuwa namba 105, 2021 lililokuwa likiwakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Katika rufaa hiyo waomba rufaa hao walikuwa wakilishwa na Mawakili Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Sylvster Kahunduka, Edmund Ngemela na Fridolin Bwemelo ambao kwa pamoja walipinga hoja za wajibu rufaa na kuomba mahakama iridhie hoja zao 14 za rufaa na kuwaachia wateja wao huru.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu