Daktari wa soka Zambia afariki dunia baada ya mchezo wa Nigeria na GhanaMmoja wa madaktari bingwa wa Zambia amefariki dunia baada ya mchezo wa Nigeria dhidi ya Ghana wa kufuzu Kombe la Dunia Jumanne usiku, wakati mashabiki wa Nigeria walipoanza kuwashambulia wachezaji na wafanyakazi wa Ghana uwanjani na kusababisha tafrani au mkanyagano.


Haijabainika jinsi Dk. Joseph Kabungo alivyofariki - kuna baadhi ya ripoti kwamba alipatwa na mshtuko wa moyo.

Alikuwa mmoja wa madaktari wa mechi hiyo mjini Abuja wakati Nigeria ilipotoka sare na wapinzani wao 1-1, na kupelekea Ghana kufuzu kulingana na sheria ya bao la ugenini.


Matukio mabaya yalifuata baada ya mashabiki wa Super Eagles waliokuwa na hasira kushambulia timu pinzani kwa chupa za maji zilizorushwa kutoka jukwaani walipokuwa wakiondoka uwanjani, huku polisi wakiripotiwa kutumia vitoa machozi kuwatawanya umati huo.


Mamlaka ya Nigeria bado haijasema lolote hadharani kuhusu tukio hilo.


Daktari huyo alikuwa mchezaji wa kudumu katika mechi kuu za soka, ikiwa ni pamoja na Kombe la hivi karibuni la Fifa Arab Cup nchini Qatar na Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Cameroon.


Kifo chake ambacho hakikutarajiwa kimewaacha wadau wa soka wa Zambia katika huzuni.


“Tunatuma rambirambi zetu za dhati kwa familia ya Dk. Kabungo na familia ya soka kwa ujumla,” rais wa FA wa Zambia Andrew Kamanga alisema katika taarifa yake kuthibitisha kifo hicho.


Gwiji wa soka wa Zambia Kalusha Bwalya, ambaye alikuwa marafiki wa karibu na Bw Kabungo alishtuka, akiambia BBC kuwa haamini habari hizo.


Dk. Kabungo alikuwa daktari wa timu ya taifa wakati nchi hiyo ya kusini mwa Afrika iliponyanyua taji lao la kihistoria la Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.


Pia alikuwa sehemu ya kamati ya matibabu ya Fifa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) wakati wa kifo chake.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu