Chadema wadai wataanza mikutano yao iliyozuiwaWakati Kikosi Kazi cha kukusanya maoni ya watu kuhusu mfumo wa demokrasia wa vyama vingi nchini kikiendelea kupokea maoni hayo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitaanza kuifanya mikutano ya hadhara iliyozuiwa.


Chadema hakina mjumbe kwenye Kikosi Kazi hicho na hakikwenda kupeleka maoni yake kama vilivyofanya vyama vingine vya siasa.


Licha ya kutoshiriki kwenye Kikosi Kazi hicho, ujumbe wa Chadema ukiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe siku chache zilizopita walikutana na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na wajumbe kutoka CCM na serikalini kuzungumzia masuala mbalimbali, ikiwemo maridhiano ya kisiasa.


Juzi Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es salam kuwa hakuna sababu ya kudhibitiana kwa mfumo na njia zisizo rasmi.


Alisema msimamo wa chama utabaki palepale kwamba hawatashiriki mchakato wowote ambao hauwezi kujenga, kuinua wala kuimarisha demokrasia na haki za Watanzania.


“Dhima ambayo Chadema tunaibeba mbele ya Watanzania, mnajua hitaji lililo na matumaini mbele ya Chadema, hatuko tayari kuvuruga imani hiyo wala hitaji hilo kwa namna yoyote ile.


“Kama walivyoitisha kikao hicho bado tunaamini, sio kwamba hakuna haja ya utungwaji wa kanuni ya kusimamia mikutano ya hadhara hapa nchini, bali kufanya hivyo ni kupoteza muda wa wananchi na kutengeneza sintofahamu ndani ya nchi yetu,” alisema.


Alisema kinachoitwa kanuni walizipokea kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ikiwa na mambo 10 ambayo walitaka kutoa maoni na kuwasilisha kwenye kikao hicho juu ya kinachoitwa kanuni ya kuongoza mikutano ya Vyama vya Siasa.


“Ukiangalia yale mambo 10 yaliyoorodheshwa kwenye randama, hakuna jambo ambalo halipo, mambo yote yapo, mara kuna kanuni za miongozo, usimamizi wa miongozo ya vyama vya siasa humo ndani yote yapo,” alisema.


Mwalimu alisema hakuna asiyefahamu mikutano inaanza saa ngapi na kuisha saa ngapi, nakupendekeza mikutano kuanza na kumalizika kulingana na jua linavyozama kwenye eneo hilo.


“Hata kama hiyo nia njema ingekuwepo, angalau tungeona kwenye vipengele ambavyo vinahitaji maboresho ya vyama vya siasa, lakini bado wamekuwa wakisisitiza mwisho wa mikutano ni saa 12 jioni.”


Akizungumzia suala la vibali vya kufanya mikutano, alisema Jeshi la Polisi lina watu wasio waaminifu na weledi, ambapo kwenye randama hiyo imeainishwa.


Hata hivyo, jana si Msajili wa Vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi wala msaidizi wake Sisty Nyahoza waliopatikana kuzungumzia suala hilo kwa simu.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu