Askari polisi adaiwa kumuua mkewe kwa wivu wa mapenzi DodomaPolisi mkoani Dodoma wametangaza kumshikilia mfanyabiashara, Peter Mwakiposile (45) mkazi wa Kikuyu Chidachi jijini humo kwa tuhuma za kumuua mkewe Aisha Ramadhan (39) kwa kipigo chanzo kikitajwa ni wivu wa mapenzi.


Kamanda wa Polisi mkoani humo, Martine Otieno alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi Mtaa wa Kikuyu Chidachi.


Alisema mtuhumiwa alimpiga Aisha sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia fimbo na kumsababishia maumivu makali.


Kamanda Otieno alisema majirani walimchukua Aisha na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya General na alifariki dunia muda mchache wakati akitibiwa.


“Huyo mume wake tumemtafuta usiku huohuo wa jana(juzi), tumempata na tupo naye kwa hiyo tunaendelea na upelelezi ili kukamilisha jalada letu na sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema Kamanda Otieno.


Alipoulizwa mtuhumiwa anafanya shughuli gani, kamanda Otieno alisema ni mfanyabiashara.


Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri alisema mtuhumiwa huyo pia amewahi kuwa askari polisi.


“Nilipewa hizo taarifa na kulikuwa na hofu kwamba aliyehusika ni askari na askari walikuwa wanataka kuficha upungufu uliojitokeza mpaka huyo mama akafariki dunia,” alisema Shekimweri.


“Actually’ huyo bwana alikuwa anataka kutoroka tulielekeza watu wetu na polisi walilishughulikia hilo jambo na huyu bwana amekamatwa na tunavyoongea yupo katika mikono ya sheria.”


Alisema alikuwa na taarifa kwamba wanandoa hao wamekosana na wamekuwa wakipigana mara kwa mara.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu