Aliyesusa kujitetea mahakamani ahukumiwa miaka 30 gerezaniMahakama ya Wilaya ya Temeke imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mkazi wa Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, Said Issa baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.


Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Jimson Mwankenja, aliyesikiliza kesi hiyo baada ya kuridhika na ushahidi wa mashtaka.


Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka pekee kwa kuwa mshtakiwa alizira kujitetea baada ya hakimu Mwankenja kukataa kujitoa katika kesi hiyo.


Awali ilidaiwa kuwa Februari 15, 2021, eneo la Mkwamba, Temeke, aliiba simu aina ya Infinix mali ya Neema Masinde.


Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi watatu, akiwemo Neema mwenyewe na kuwasilisha vielelezo vinne, huku ikidaiwa kabla ya kupora simu hiyo, mshtakiwa alimjeruhi Neema kwa kisu mkononi na shingoni.


Mei 25, 2021 mahakama ilimuona mshtakiwa kuwa ana kesi ya kujibu na hivyo akapewa haki ya kujitetea, ndipo akasema atajitetea mwenyewe.


Julai 14, 2022, aliomba ahirisho ili apewe mwenendo wa kesi na alipokataliwa akamtaka hakimu ajiondoe kwenye kesi hiyo.


Ombi hilo lilikataliwa kwa kuwa hakuwa ametoa sababu za kumfanya ajiondoe, hivyo akazira kujitetea.


Kufuatia hatua hiyo, mahakama ikatoa kifungo cha miaka 30 jela.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu