Ahojiwa baada ya kudai Polisi wamempora mali zake
Jeshi la Polisi limeanza kuuchunguza malalamiko ya mfanyabiashara wa Kilombero aliyedai kuteswa, kunyang’anywa pesa na mali zake na askari baada ya kukamatwa kwa tuhuma za wizi.


Maofisa watatu kutoka Makao Mkuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma, walimhoji Galus Yondani (41) Ijumaa iliyopita mjini Morogoro baada ya gazeti hili kuchapisha habari juu ya kilio chake wiki iliyopita.


Timu ya polisi ikiongozwa na Kamshna wa Polisi, Ulomi ilifanya mahojiano na Yondani katika Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro kwa takriban saa tano kuanzia saa nane mchana.


Yondani alikamatwa Agosti 8 mwaka 2020 na askari polisi watatu akiwa Chalinze mkoani Pwani akielekea Kilombero anakoishi na kufanya biashara zake.


Askari hao walikuwa wakichunguza wizi wa Sh159 milioni katika duka la vinywaji vikali mkoani Singida linalomilikiwa na mfanyabiashara wa Dodoma, Alex Lupingo.


Yondani alidai baada ya kukamatwa, askari hao walimtesa wakitaka awaeleze iwapo anamfahamu Yohana Lupingo ambaye ni mdogo wa Alex aliyekuwa akisimamia duka la kaka yake huko Singida.


Alidai akiwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, askari walimtesa na saa 12:45 jioni walimlazimisha atoe namba yake ya siri ya benki.


Alidai baada ya kuteswa aliwapa namba ya siri waliyoitumia kuhamisha kiasi cha Sh1 milioni kutoka kwenye akaunti yake na kuzituma kwenye namba yake ya simu kabla ya kuzituma tena kwenye namba nyingine na kuzitoa.


Kijana huyo alidai askari hao walichukua mifuko 443 ya simenti katika duka lake huko Kilombero, pikipiki mbili na gari aina ya Toyota Noah na fedha taslimu Sh5.3 milioni alizokuwa amezihifadhi kwenye begi lake ndani ya gari.


Kwa mujibu wa Yondani, hadi wiki iliyopita alikuwa hajarudishiwa mali zake zikiwamo kadi ya benki licha ya mahakama kumwachia yeye na wenzake katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili. Mahakama ya Wilaya ya Singida iliamuru warudishiwe mali zao.


Jana, Yondani alisema baada ya mahojiano marefu, timu hiyo ya polisi ilimhakikishia kuwa mali zake zote zimehifadhiwa Kituo Kikuu cha Polisi Singida kama vielelezo vya kesi na kuahidi atarudishiwa pesa zake watakapomaliza uchunguzi.

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu