Mamia ya wafungwa watoroka jela nchini Libya


Mamia ya wafungwa waliokuwa wamefungwa jela katika mji wa Surman wa magharibi mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, wametoroka jela na kukimbilia kusikojulikana.

Televisheni ya "Rusia al Yaum" imetangaza habari hiyo ikiinukuu Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na kusema kuwa, wafungwa 393 waliokuwa wanashirikiliwa jela huko Surman walitoroka jela jana Jumatano wakati askari wa serikali walipokuwa wanausafisha mji huo kutokana na uwepo wa wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar. Wafungwa hao walitumia fursa ya kukosekana ulinzi wa kutosha kutoroka jela na kukimbilia kusikojulikana.

Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya imewataka wafungwa hao kujisalimisha kwa taasisi husika kama ambavyo imetoa amri kwa wanajeshi wake kuhakikisha wafungwa wote wanakamatwa tena na kurudishwa jela.

Askari wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya juzi Jumanne waliukomboa kikamilifu mji wa Surman kutoka mikononi mwa jenerali muasi, Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri.

Hakuna ishara zozote za kumalizika vita vya ndani nchini Libya

Umoja wa Mataifa umetahadharisha vikali kuhusu madhara ya kuendelea mapigano nchini Libya badala ya nguvu za nchi hiyo kuelekezwa kwenye vita dhidi ya corona.

Siku chache zilizopita na katika hali ambayo, mashambulio ya maroketi ya wanamgambo watiifu kwa jenerali muasi Khalifa Haftar dhidi ya mji mkuu Tripoli yakiwa yanaendelea, Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj ilitangaza siku ya Jumatatu kwamba, imefanikiwa kuikomboa miji minane ya magharibi mwa Tripoli iliyokuwa ikidhibitiwa na wanamgambo hao wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya.

Muhammad Qanunu, msemaji wa vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya alitangaza katika taarifa yake kwamba, baadhi ya miji iliyokombolewa na vikosi vyao ni Surman, Sabratah, al-Ajital, al-Jumayl na Riqdalin.

www.mzunguko.com

\


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu