Kitendo cha Marekani cha kuikatia misaada WHO ni jinai dhidi ya binadamu


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameelezea kusikitishwa kwake na hatua ya rais wa Marekani ya kulikatia misaada ya kifedha Shirika la Afya Duniani (WHO) tena wakati huu wa mapambano ya dunia nzima dhidi ya corona na kusema kuwa, hatua hiyo ya Marekani ni ushahidi mwingine wa wazi kwamba viongozi wa nchi hiyo ni watenda jinai dhidi ya binadamu.

Juzi Jumanne, rais wa Marekani, Donald Trump alisimamisha misaada ya kifedha ya nchi hiyo kwa Shirika la Afya Duniani, (WHO).

Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana Jumatano alilaani jinai hiyo ya viongozi wa Marekani na kusema kuwa, kitendo hicho ni hatua nyingine ya kudhoofisha ushirikiano wa kimataifa katika kutatua masuala ya dunia.

Amesema, masuala ya afya, amani na usalama wa roho za watu duniani uko hatarini moja kwa moja hivi sasa kutokana na maambukizi makubwa ya corona, lakini Marekani imeamua kuiadhibu taasisi ambayo ndiye mratibu pekee wa masuala ya matibabu duniani katika wakati huu mbaya sana ambapo dunia nzima inalihitaji mno shirika hilo katika kupambana na janga la ulimwengu mzima la corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO)

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amesema, lengo kuu la Donald Trump la kulikatia misaada Shirika la Afya Duniani WHO ni kuficha uzembe na kushindwa serikali yake kudhibiti maambukizi ya corona ndani ya Marekani. Hivyo ameitaka jamii ya kimataifa kusimama imara kwa pamoja kukabiliana na siasa hizo mbovu za Marekani na kutoiacha mkono WHO.

Amekumbusha kuwa, wanasiasa wa Marekani wanapaswa kuelewa kwamba, hatua yao hiyo ni uvunjaji wa wazi wa ahadi zao kwa jamii ya kimataifa na hawawezi kuziteka juhudi za kimataifa za kusaidia binadamu kupitia kulikatia misaada na kulishinikiza shirika hilo la afya duniani.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu