Watu 18 waaga dunia katika ajali ya barabarani Tanzania


Watu 18 wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa baada ya magari mawili kugongana katika kijiji cha Kilimahewa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, mashariki mwa Tanzania.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rufij, Onesmo Lyanga ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa, ajali hiyo imehusisha lori na gari la abiria aina ya Toyota Coaster. Amesema,

"ni kweli ajali hiyo imetokea mapema leo asubuhi na imesababisha vifo vya watu 18 na majeruhi 15."

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi la Tanzania ameongeza kuwa, ajali hiyo imetokea baada ya Coaster iliyokuwa ikitokea mikoa ya Kusini kwenda Dar es Salaam kugongana na lori lililokuwa likitokea Kimanzichana.

Kamanda huyo wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Rufij, Onesmo Lyanga amesema majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa katika kituo cha kiafya cha Kilimahewa.

Visa vya ajali za barabarani vimeongezeka Tanzania

Katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa ikikumbwa na ajali za barabarani na ambazo zimesababisha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha.

Septemba mwaka jana, watu 15 walipoteza maisha na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika mkoa wa Mbeya, kusini mwa Tanzania, miezi michache baada ya watu wengine 14 kufariki dunia katika ajali nyingine iliyotokea mkoani Pwani.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu