WHO: Visa vya maambukizi vyapungua Italia na Uhispania

April 15, 2020

Shirika la afya duniani limesema kuwa visa vya maambukizi ya virusi vya Corona vinapungua nchini Italia na Uhispania tofauti na Uingereza, Uturuki na Marekani ambapo visa vya maambukizi vinazidi kuongezeka.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus

 

Shirika la afya duniani WHO limesema asilimia 90 ya visa vipya vya maambukizi ya virusi vya Corona kwa sasa hivi vinatokea Ulaya na Marekani na wala sio China, ambayo ilikuwa kitovu cha maambukizi ya virusi hivyo.

 

Msemaji wa WHO daktari Margaret Harris amesema hayo akiwa Geneva na kuongeza kuwa visa vipya vya maambukizi nchini China vinaletwa na wageni.

 

Vile vile amesema ulimwengu usitarajie chanjo dhidi ya virusi vya Corona katika muda wa mwaka mmoja au hata zaidi.

 

Naye katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami NATO Jens Stoltenberg amezitaka nchi wanachama wa muungano huo kuchukua janga la virusi vya Corona kama funzo ili kuongeza vifaa vya matibabu badala ya kutegemea misaada ya nje.

 

Stoltenberg amesema hayo siku moja tu kabla ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wa Nato utakaofanyika kwa njia ya video.

 

Amesema mkutano huo utajikita zaidi katika suala la kuongeza ushirikiano kati ya nchi wanachama hasa kwa usafirishaji wa vifaa vya matibabu kwa sehemu zinazohitajika zaidi.

Rais wa Iran Hassan Rouhani

 

Nchini Iran, idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 imepungua kwa mara ya kwanza mwezi huu.

 

"Tumeweka vikwazo vya usafiri kati ya wilaya moja hadi nyIngine kote nchini. Mungu akipenda, tunapanga kuondoa vikwazo hivyo ifikapo Aprili 20" amesema Rais wa Iran Hassan Rouhani.

 

Msemaji wa wizara ya afya nchini humo Kianoush Jahanpour amesema kuwa watu 98 wamekufa kutokana na ugonjwa wa COVID 19 katika muda wa saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya watu waliofariki kwa ugonjwa huo kuwa 4,683.

 

Jahanpour ameongeza kuwa watu wengine 1,574 wamepatikana na virusi vya Corona na kufikisha idadi jumla ya watu walioambukizwa virusi hivyo kuwa 74,877.

 Na nchini Uhispania na Austria, mamlaka zimeruhusu japo kwa kadri watu kuanza kurudi kazini kinyume na Ufaransa na India ambazo zimerefusha muda wa usitishaji wa shughuli ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona.

 

Nchini Uhispania, vikwazo vimesaidia kupunguza kasi ya maambukizi na idadi ya vifo ambavyo vilikuwa vimefikia kilele chake mapema mwezi huu wa Aprili. Nchi hiyo imerekodi idadi ndogo ya maambukizi mapya tangu Machi 18.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon