Vikosi vya serikali ya Libya vyakomboa miji minane iliyokuwa ikishikiliwa na wapiganaji wa Haftar


Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya (GNA) imetangaza kuwa vikosi vyake vimekomboa miji minane iliyokuwa ikidhibitiwa na wapiganaji watiifu kwa jenerali muasi Khalifa Haftar.

Msemaji wa GNA Muhammad Gnunu amesema katika taarifa aliyotoa jana kwamba, vikosi vya serikali hiyo vimeikomboa miji ya Surman, Sabratha, al-Ujailat, al-Jumail, Raqdalin, Zaltan, al-Aasa na Melita kusini mwa Tripoli, mji mkuu wa nchi hiyo.

Gnunu ameongeza kuwa, vikosi vya serikali vinawaandama wapiganaji wanaokimbia wa vikosi vya Haftar huku vikiendelea kusonga mbele, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa operesheni ya 'Dhoruba ya Amani' iliyoanza Machi 26 kwa lengo la kukabiliana na hujuma na mashambulio yaliyoanzishwa na wapiganaji watiifu kwa Haftar dhidi ya Tripoli.

Msemaji huyo wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya amebainisha kuwa, ushindi huo wa kijeshi viliopata vikosi vya GNA vimeiwezesha serikali hiyo kudhibiti barabara inayoanzia kwenya mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Tunisia hadi eneo la Abu Qurain kusini mashariki mwa Tripoli.

Kiongozi wa GNA, Fayez al-Sarraj (kulia) na kiongozi wa LNA Khalifa Haftar

Wakati huohuo vikosi vya kundi linaloongozwa na Khalifa Haftar linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) vimetangaza leo kuwa, vimeiangusha ndege nyingine isiyo na rubani ya Uturuki kusini mwa Tripoli, ambayo iliruka kutokea kituo cha jeshi cha Muaitiqah.

Watu zaidi ya 1,500 wameuawa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, wengine wasiopungua 6,000 wamejeruhiwa na zaidi ya laki moja na nusu wamebaki bila makazi tangu vikosi vinavyoongozwa na Haftar na kuungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi vilipoanzisha hujuma na mashambulio mwezi Aprili mwaka jana kwa lengo la kuuteka mji mkuu huo wa Libya unaodhibitiwa na serikali ya Muafaka wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu