Waafrika 111 waishio Guangzhou, China wabainika kuambukizwa virusi vya corona

April 14, 2020

Jumla ya raia 111 wa nchi za Kiafrika wanaoishi katika mji wa Guangzhou ulioko kusini mwa China wamebainika kuwa wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la China, Xinhua.

 

Likimnukuu Chen Zhiying, ambaye ni Naibu Mtendaji wa Meya wa Guangzhou, shirika hilo la habari la China limeripoti leo kuwa, kwa mujibu wa takwimu, hadi kufikia jana raia 111 wa nchi za Kiafrika, wakiwemo 19 ambao ni wasafiri waliongia na virusi hivyo kutoka nje ya China wamebainika kuwa na virusi vya corona.

 

Chen ameongeza kuwa, tangu Aprili 4 hadi sasa, jumla ya raia 4,553 wa nchi za Kiafrika wanaoishi katika mji wa Guangzhou wamepimwa ili kujua kama wameambukizwa COVID-19 au la.

 

Hapo jana, China ilitupilia mbali madai ya wanadiplomasia wa nchi za Afrika na Marekani kwamba mamlaka za nchi hiyo zinaamiliana vibaya na raia wa kigeni katika mji huo wanaoonekana kuwa ni Waafrika, ikiwa ni pamoja na kuwalazimisha kupima virusi vya corona na kuwaweka karantini kwa nguvu.

Raia wa Kiafrika inaosemekana wananyanyaswa na kubaguliwa nchini China

 

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitoa taarifa ya kukemea vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi dhidi ya Waafrika wanaoishi katika jimbo la Guangdong ulipo mji huo wa Guangzhou na kusisitiza kuwa, serikali ya Beijing itaendelea kuhakikisha raia wote wa kigeni wanapatiwa haki sawa nchini humo.

 

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya video na picha kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha Waafrika wengi wakiwa wamezagaa mitaani katika maeneo mbalimbali nchini China wakiwa na mabegi ya nguo, wakidai wamefukuzwa kwenye nyumba zao na mahotelini.

 

Taarifa zaidi zimedai kwamba, vitendo hivyo vya ukiukaji haki za binadamu vimekuwa vikifanywa na mamlaka za serikali ya China ambazo zinawashutumu raia wa kigeni hususan Waafrika kwamba wanasambaza ugonjwa wa COVID-19 nchini humo.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon