Corona yailazimisha Tanzania kupiga marufuku safari za ndege

Hatimaye serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga marufuku safari zote za ndege za abiria za kimataifa.

Akitangaza rasmi mafuruku hiyo, Msemaji Mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tannzaia, Hassan Abbas ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwamba, hiyo ni hatua nyingine ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Msemaji Mkuu wa Serikali@TZMsemajiMkuu

Mamlaka ya Usalama wa Anga nchini imefuta safari za ndege zote za abiria za kimataifa na kuweka vikwazo zaidi kwa ndege maalum za mizigo zitakazoruhusiwa kutua nchini. Hii ni hatua nyingine ya kupambana na Ugonjwa wa Covid-19.

Nayo Mamlaka wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema kuwa, kuanzia tarehe 11 Aprili 2020 ndege zote za kimataifa za abiria ambazo zilikuwa na ratiba ya kutua na hata ambazo hazikuwa na ratiba ya kutua Tanzania zimepigwa marufuku kutua.

Itakumbukwa kuwa nchi jirani na Tanzania kama Rwanda na Kenya zilichukua hatua zamani za kuzuia maambukizi ya kirusi cha corona. Mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili, Kenya iliongeza muda wa marufuku ya ndege za kimataifa kutua nchini humo kwa siku 30 zaidi.

Hali ya kuchanganyikiwa yaigubika Marekani huku mamia kwa mamia ya watu wakifariki dunia kila siku kwa corona.

Ikumbukwe kuwa nchi 52 za Afrika zimekumbwa na ugonjwa wa COVID-19 huku taarifa za karibuni kabisa zikisema kuwa, zaidi ya watu 13,600 barani Afrika wameshaambukizwa ugonjwa huo, watu 742 wameshafariki dunia na wengine 2,358 wameshapata afueni baada ya kuugua ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi.

Nchi inayoongoza kwa wagonjwa wengi na vifo vingi zaidi vya corona duniani ni Marekani. Hadi leo asubuhi, zaidi ya watu 560,433 walikuwa wameshathibitishwa kuugua corona nchini Marekani na zaidi ya 22,115 walikuwa wameshafariki dunia.

Ugonjwa wa COVID-19 umeshaenea dunia nzima huku idadi ya walioambukizwa corona kote duniani kufikia leo asubuhi ilikuwa ni zaidi ya watu 1,853,155, waliofariki dunia walikuwa ni zaidi ya 114,247 na waliopata afueni ni zaidi ya 423,625.

Ukitoa Marekani, nchi tano kubwa za Ulaya za Uhispania, Italia, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ndizo zinazoongoza duniani kwa idadi kubwa zaidi ya maambukizi na vifo cha corona. Vifo vya COVID-19 katika nchi hizo tano kubwa za Ulaya ni zaidi ya nusu ya vifo vyote vya corona kote ulimwenguni.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu