Vikosi vya serikali ya Libya vyaripua ndege yenye shehena ya silaha ya kundi la Khalifa Haftar


Vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya (GNA) vimeiteketeza ndege moja iliyokuwa imebeba shehena ya silaha na zana za kijeshi kwa ajili ya kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar.

Kundi la LNA limetangaza kuwa, vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa jana viliishambulia ndege ya mizigo iliyokuwa imebeba shehena ya silaha na zana za kijeshi kwa ajili ya kundi hilo.

Ripoti zinasema, vikosi vya GNA inayoongozwa na Fayez al-Sarraj viliishambulia ndege hiyo mara baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Tarhuna.

Taswira za tukio hilo zilizochukuliwa kutokea kando kando ya uwanja huo wa ndege zimeonyesha moshi mzito unaofuka na kupaa angani; na kwa mujibu wa baadhi ya duru moto ulioteketeza shehena hiyo ya silaha uliendelea kuwaka kwa saa kadhaa.

Ijapokuwa nchi ilikotoka ndege hiyo ya mizigo haijatangazwa lakini sehemu kubwa ya silaha zinazotumiwa na kundi la LNA linaloongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar inadhaminiwa na Imarati, Misri na Saudi Arabia.

Aprili 2019, vikosi vya Haftar vilianzisha hujuma na mashambulio dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa lengo la kuuteka mji huo unaodhibitiwa na vikosi vya serikali ya muafaka wa kitaifa.

Licha ya mripuko wa virusi vya corona vilivyosambaa duniani pamoja na miito ya jamii ya kimataifa ya kutaka kusitishwa vita, pande hasimu nchini Libya zingali zinaendelea kupambana na kushambuliana.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ulitoa taarifa siku ya Jumamosi kwa mnasaba wa kuwadia Aprili 4, siku yalipoanza mashambulio ya vikosi vya Haftar dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo na kueleza kwamba, katika mwaka mmoja uliopita tangu yalipoanza mashambulio ya vikosi vya mashariki ya Libya vilivyo chini ya uongozi wa Khalifa Haftar dhidi ya Tripoli raia 356 wameuawa, 326 wamejeruhiwa na watu wengine wapatao 149,000 katika mji mkuu wa Libya na vitongoji vyake wamebaki bila makazi.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu