Uganda yatakiwa kuheshimu haki za binadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limeitaka serikali ya Uganda kuhakikisha kuwa vikosi vyake vya usalama vinajiepusha kutumia nguvu wakati wa kutekeleza hatua za kukabiliana na janga la COVID-19.

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch katika ripoti yake limevitaka vikosi vya kulinda usalama nchini Uganda kujiepusha kutenda vitendo vya ukatili dhidi ya raia wa Uganda.

Kulingana na mtafiti wa Uganda kwenye shirika la Human Rights Watch Oryem Nyeko, vikosi vya usalama vimekuwa vikitumia nguvu nyingi kutekeleza hatua za serikali zilizowekwa kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Nyeko amesema wakati ambapo Uganda pia inapokabiliwa na changamoto ya kiafya ni muhimu zaidi kwa

serikali kuhakikisha kuwa haisababishi visa vya kukiukwa haki za binadamu.

Hadi kufikia sasa watu 44 wamethibitishwa kuambukizwa na virusi vya corona na hakuna mtu yeyote aliyefariki mpaka sasa. Serikali ya Uganda imeongeza hatua zaidi kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Mnamo Machi 25 serikali ya Uganda ilipiga marufuku shughuli za usafiri wa umma na masoko yasiyokuwa ya chakula. Kabla ya hapo ilianzisha hatua za lazima za kuwaweka watu karantini walioingia nchini humo kutokea nje katika hoteli ambazo walitakiwa kujilipia gharama zote.

Wiki moja baadae Rais Yoweri Museveni alitangaza hatua kadhaa za nyongeza, ikiwa ni pamoja na marufuku ya kutembea nyakati za usiku kwa muda wa siku 14.

Siku iliyofuata, Richard Karemire, msemaji wa jeshi la Uganda, alitangaza kwamba jeshi, na polisi wenye silaha wa Kitengo cha Ulinzi wa Mitaa (LDU), kinachoshirikiana na jeshi la Uganda, kitafanya doria na kusaidia kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na serikali.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu