Mgogoro wa sasa wa virusi vya corona ndio mbaya zaidi duniani tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa maambukizi ya sasa ya virusi vya corona ndiyo mgogoro mkubwa zaidi duniani tangu baada ya vita vya Pili vya Dunia.

Antonio Guterres ameyasema hayo huku idadi ya watu walioaga dunia kutokana na virusi vya corona nchini Marekani ikizidi ile ya wahanga wa virusi hivyo nchini China. Idadi ya watu waliopatwa na virusi hivyo kote dunia sasa imepita 860,000.

Jumanne ya jana peke yake Marekani ilitangaza vifo vya watu 800 kutokana na virusi vya corona, suala linaloifanya idadi ya Wamarekani walioaga dunia kutokana na virusi hivyo kufikia zaidi ya 4,055.

Kaimu Waziri wa Jeshi la Majini la Marekani, Thomas Moodley ametangaza kuwa, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon inafanya jiihada za kuwahamisha wanajeshi waliopo kwenye manuwari ya vita ya Theodore Roosevelt na kuwapeleka katika kisiwa cha Guam baada ya virusi vya corona kuwakumba maafisa wa jeshi hilo.

Matamshi hayo ya Moodley yametolewa baada ya vyombo vya habari vya Marekani kufichua barua iliyotumwa na nahodha wa manuwari ya vita ya Theodore Roosevelt kwa Pentagon akiomba wanajeshi zaidi ya elfu nne waliko kwenye manuwari hiyo kuhamishiwa sehemu nyingine baada ya zaidi ya wanajeshi mia moja kukumbwa na virusi vya corona.

Maelfu ya Wamarekani wameaga dunia kutokana na virusi vya corona

Wakati huo huo Waziri ya Mambo ya Nje ya Marekani, Mike Pomeo ametangaza kifo cha afisa wa ngazi ya juu wa wizara hiyo kutokana na corona. Pompeo hakutaja wasifu, cheo wala mahali mwanadiplomasia huyo alipofia.

Virusi hivyo pia vimeendelea kuweka rekodi mpya katika nchi za Ulaya kwa kuua idadi kubwa zaidi ya watu katika siku moja tangu vianze kusambaa katika nchi hizo.

Nchi za Uhispania, Uingereza, Ufaransa na Italia zimesajili kiwango cha juu zaidi cha vifo vya watu kutokana na virusi vya corona hiyo jana tangu mlipuko wa virusi hivyo ulipoanza. Watu 12,428 wameaga dunia nchini Italia peke yake kutokana na virusi hivyo na suala hilo linaifanya kuwa nchi yenye wahanga wengi zaidi wa janga hilo duniani.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu