Marekani yaongoza maambukizi ya COVID-19, China yatangaza ushindi

Maambukizi ya kirusi cha corona yamepindukia 100,000 nchini Marekani na kulifanya taifa hilo kuongoza duniani, katika wakati ambapo China, ambayo ilianza kuwa na wagonjwa wa mwanzo ikitangaza kukidhibiti kirusi hicho.

China inasema kuna wagonjwa wapya 31 wa ugonjwa wa COVID-19 na vifo vinne hivi leo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kamisheni ya Afya ya nchi hiyo.

Miongoni mwa wagonjwa hao 31, thalathini walitoka nje ya nchi hiyo, na ni mmoja tu aliyeambukizwa katika jimbo la kaskazini magharibi la Gansu.

Wanne waliofariki dunia ni kwenye jimbo la Hubei, kiini cha maambukizi ya kirusi cha corona, ambalo hata hivyo halina mgonjwa mpya. Jimbo hilo lililokuwa kwenye marufuku ya kutotoka nje, limeanza kurejea kwenye maisha yake ya kawaida.

Maambukizi kutoka nje ndicho kikwazo kikubwa kwa China kwa sasa, baada ya hapo jana Baraza lake la Taifa kutangaza kwamba kimsingi nchi hiyo imefanikiwa kuuzuwia ugonjwa wa COVID-19.

Tangu kirusi hicho kianze kusambaa mwezi Disemba mwaka jana, watu 81,470 wameambukizwa nchini China pekee, ambako 3,304 wamepoteza maisha.

Rais Donald Trump wa Marekani

Nchini Marekani, idadi ya walioambukizwa imefikia 142,000, huku waliopoteza maisha wakipindukia 2,500.

Katika jimbo la New York pekee, watu zaidi ya 1,000 wameripotiwa kufa, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu mgonjwa wa mwanzo kugundulika kwenye jimbo hilo.

Kufikia jioni ya jana, eneo la mjini la jimbo hilo lilitangaza kuwa vifo vimefikia 776, huku miji mingine ikitangaza vifo 250, na hivyo kuifanya idadi kamili ya waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi hicho kufikia 1,026.

Hayo yanakuja wakati Rais Donald Trump akitangaza kwamba huenda vifo vyote vitavyotokana na kirusi hicho vikapindukia 100,000 nchini Marekani. Trump ameongeza muda wa watu kujitenga ili kuepuka maambukizi mapya hadi tarehe 30 mwezi Aprili.

Muda wa awali uliowekwa ulikuwa wa wiki mbili, ambao unamalizika leo.

WWW.MZUNGUKO.COM


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu