Jeshi la Somalia lawaua magaidi 142 wa kundi la Al-Shabab, lakomboa Janale


Jeshi la Somalia (SNA) limetangaza kuwa limewaua magaidi wapatao142 wa kundi la al-Shabaab, wamewajeruhi 29 na wengine 18 wamekamatwa kwenye operesheni iliyofanyika katika mji wa Janale, kusini mwa Somalia.

Kamanda wa jeshi hilo Osman Shabel amesema wanajeshi waliukomboa tena mji wa Janale kutoka kwa magaidi hao wakufurishaji wenye mfungamano na al-Qaeda wiki mbili zilizopita. Ameongeza kwamba hakuna majeruhi kwa jeshi la Somalia, na wanajeshi hao walizirejesha familia zilizoondolewa kwenye nyumba na kuwapa chakula.

Jeshi la Somalia limekuwa likiwalenga magaidi wa Al-Shabaab katika eneo la Lower Shabelle katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Siku chache zilizopita, magaidi 12 wa al-Shabaab waliangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia katika eneo la Bay, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Haya yanajiri siku tatu baada ya vikosi vya jeshi la serikali vikishirikiana na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM) kuua magaidi sita wa al-Shabaab katika operesheni dhidi ya maficho ya magaidi hao katika vijiji vya eneo la lower,Juba Kusini mwa nchi.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Umoja wa Mataifa unafadhili askari hao wa AMISOM ambao sasa ni 21,000 na wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007. Wanajeshi wa Amisom walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu