Uchaguzi wa marudio nchini Malawi sasa kufanyika Julai Pili


Uchaguzi wa marudio kwa ajili ya kiti cha urais nchini Malawi umepangwa kufanyika tarehe Pili ya mwezi Julai mwaka huu.

Uchaguzi huo unarejewa baada ya Mahakama ya Katiba nchini humo kubatilisha matokeo yaliyompa ushindi Rais Peter Mutharika.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Malawi Jane Ansah amewaambia waandishi wa habari kwamba, “kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Katiba wa Februari 3 uliofuta matokeo ya uchaguzi wa Rais na kuagiza kufanyika uchaguzi mpya kwa sababu ya dosari, natangaza kwamba, uchaguzi mkuu utafanyika Julai Pili.”

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo ilisema kuwa, matokeo ya uchaguzi huo kwa kiasi kikubwa yaligubikwa na udanganyifu na hivyo kuagiza kurejewa katika kipindi cha siku 150.

Hata hivyo Rais Peter Mutharika alipinga hukumu hiyo na kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba ya Malawi ambao ulimvua madaraka kwa kubatilisha ushindi wake.

Katika hoja zake Rais Mutharika alidai kwamba, hukumu hiyo ilikuwa ni upotoshaji wa haki na shambulio dhidi ya demokrasia nchini Malawi.

Rais Peter Mutharika wa Malawi

Hata hivyo rufaa hiyo iligonga mwamba baada ya Mahakama kutupilia mbali hoja za Rais Mutharika. Kwa mujibu wa Mahakama ya rufaa, demokrasia ni gharama hivyo wananchi wana haki ya kurudia uchaguzi.

Katika kile kinachoonekana wazi kutokubaliana na maamuzi hayo, kiongozi huyo amewasilisha rufaa yake katika mahakama ya juu zaidi ambayo imepangwa kusikilizwa Aprili 15 ya mwezi ujao kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Awali vyama vya upinzani nchini Malawi vilifungua kesi katika Mahakama ya Katiba kupinga ushindi wa Rais Mutharika kufuatia uchaguzi uliofanyika mwezi Mei mwaka jana.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu