Trump aziomba msaada wa vifaa nchi za Asia na Ulaya ili kukabiliana na corona

March 26, 2020

Gazeti la The Guardian limefichua kuwa, licha ya lugha ya mbwembwe na majigambo anayotumia Rais Donald Trump wa Marekani kwamba nchi yake haitahitaji msaada wa mataifa ya kigeni, serikali ya Washington imeomba msaada kwa waitifaki wake wa Ulaya na Asia kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona.

 

Kwa mujibu wa gazeti hilo linalochapishwa Uingereza, siku ya Jumanne, Rais Donald Trump wa Marekani alizungumza kwa njia ya simu na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini ili kuona kama nchi hiyo inaweza kuipatia Washington vifaa vya tiba kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona.

 

Ijapokuwa Ikulu ya White House haikuashiria kutolewa ombi lolote katika mazungumzo hayo, lakini Ikulu ya Rais wa Korea Kusini ya Blue House ilieleza kwamba simu hiyo ilipigwa kutokana na "ombi la haraka" la Trump.

 

 

Katika mazungumzo hayo, Trump aliusifu mpango wa upimaji virusi vya corona wa Korea Kusini ambao umesaidia kudhibiti mripuko wa Covid-19 nchini humo. Hata hivyo kwa upande wake, Rais Moon alimwambia kiongozi huyo kwamba

 

"ikiwa kuna ziada katika mahitaji ya ndani" ataafiki vifaa hivyo kupelekwa Marekani.

Kwa mujibu wa jarida la Foreign Policy, David Hale, ambaye ni mwanadiplomasia katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani ametaka apatiwe orodha ya nchi zinazoweza kuiuzia nchi hiyo "bidhaa na vifaa vya dharura vya tiba."

 

 Barua pepe iliyotumwa kwa balozi za Marekani Ulaya na Eurasia, imeeleza kuwa, kutokana na mahitaji ya dharura yaliyopo, Washington inataka kununua vifaa hivyo kwa kiwango cha mamia ya mamilioni katika nchi zote hizo ukiondoa Russia.

 

The Guardian aidha limeinukuu tovuti ya habari ya Defense One ikieleza kuwa, jeshi la anga la Marekani limeingiza kimyakimya katika mji wa Memphis pamba za pua laki tano za kufanyia vipimo vya corona kutoka Italia na kusambazwa katika maeneo mbali mbali ya Marekani.

 

Inafaa kuashiria pia kwamba, Marekani ndiyo mnunuzi mkubwa zaidi wa dawa na vifaa vya tiba kutoka China, na hivi sasa inataka kununua vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na maski za uso na vifaa vya kinga,

 

hata hivyo mazungumzo kuhusiana na mauziano hayo yametatizwa na uhasama unaoendelea kuongezeka kati ya nchi hizo mbili baada ya Trump kuendelea kung'ang'ania hadi siku za karibuni kutumia msamiati wa kibaguzi wa kukiita kirusi cha covid-19 kuwa ni "Kirusi cha China.

 

www.mzumguko.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon