Rais wa Iran kuitembelea Uganda kushiriki 'Kongamano la Kusini'


Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatazamiwa kuitembelea Uganda karibuni ili kushiriki Kongamano la Kusini.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imethibitisha habari hiyo na kusisitiza kuwa, Rais Rouhani atashiriki katika mkutano huo unaotazamiwa kufanyika jijini Kampala Aprili mwaka huu.

Hapo jana Alkhamisi, Sam Kutesa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran jijini Kampala, Sayyid Morteza Mortazavi pamoja na mjumbe maalumu wa Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran; ambapo kadhia ya mkutano huo ilijadiliwa.

Sam Kutesa (kulia) na Balozi wa Iran jijini Kampala, Sayyid Morteza Mortazavi pamoja na mjumbe maalumu wa Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu wa Uganda, Ruhakana Rugunda alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Hassan Rouhani pambizoni mwa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ambapo alimpa ujumbe wa ualishi kutoka kwa mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni aliyemualika Dakta Rouhani nchini Uganda kushiriki Duru ya Tatu ya Jukwaa la Kusini.

Jukwaa la Kusini ni tawi la juu zaidi la maamuzi la Kundi la G77. Kundi la G77 la nchi zinazostawi liliasisiwa mwaka 1964 na nchi 77, lakini hivi sasa limepanuka na lina nchi wanachama 134.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu