Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Ikulu ya Marekani yalikosoa bunge kuruhusu Trump kuchunguzwa

November 1, 2019

Ikulu ya Marekani imesema hatua ya Bunge la nchi hiyo kuidhinisha azimio la uchunguzi dhidi ya Rais Donald Trump unaokusudia kumuondoa madarakani haukuzingatia haki na kwamba ni kinyume na katiba.

Akizungumza muda mfupi baada ya azimio hilo kupitishwa, msemaji wa Ikulu ya Marekani, Stephanie Grisham amesema Trump hajafanya chochote kibaya na kwamba kitendo cha wanachama wa Democratic ni ukiukaji usiokubalika.

 

Kwa upande wake, meneja wa kampeni wa Rais Trump, Brad Parscale amesema wapiga kura watawaadhibu wanachama wa Democratic wanaounga mkono suala hilo na kwamba kiongozi huyo wa Marekani atachaguliwa tena kwa urahisi.

 

Siku ya Alhamisi, Bunge la Marekani lilipitisha azimio hilo kwa kura 232 dhidi ya 196, huku wabunge wote wa chama cha Republican wakilipinga, wakiungwa mkono na wabunge wawili wa chama cha Democratic. Azimio hilo linafungua njia ya sheria za msingi za kumchunguza rais na sio kura ya kuamua iwapo wamchunguze rais au la.

 

Huo ni ushindi kwa chama cha Democratic ambacho ndicho kinachodhibiti uchunguzi huo katika bunge. Uchunguzi huo utaangazia iwapo Trump aliishinikiza Ukraine kwa kuweka masharti ili iweze kumchunguza mpinzani wake kisiasa Joe Biden pamoja na mtoto wake wa kiume Hunter.

Afisa wa zamani wa ngazi ya juu wa Ikulu ya Marekani, Tim Morrison amethibitisha kuwa msaada wa kijeshi ulizuiwa na Trump kama sharti la kuitaka Ukraine ambayo ni mshirika wake kumchunguza Biden, lakini amethibitisha kwa mtazamo wake haikuwa kinyume cha sheria.

 

www.mzunguko.com

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload