Watu 65 wafariki dunia nchini Pakistan baada ya treni ya abiria kushika moto


Takribani watu 65 wamefariki dunia nchini Pakistan na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya kutokea moto mkubwa ndani ya treni moja ya abiria asubuhi ya leo.

Baadhi ya abiria wamepoteza maisha yao walipokuwa wakiruka katika treni hiyo kujaribu kuokoa maisha yao baada ya moto mkubwa kutanda katika baadhi ya mabehewa ya treni hiyo.

Sheikh Rashid Ahmed, Waziri wa Reli wa Pakistan amesema kuwa, tukio hilo limetokea asubuhi ya leo jirani na mji wa Liaquatpur yapata kilomita 150 kutoka katika mji wa kusini wa Multan.

Majeruhi wamepelekkwa hospitali, ingawa hapa jirani hakuna hospitali hivyo tunalazimika kuwapeleka majeruhi hao ambao baadhi yao wameungua katika hospitali za mji wa Multan kwa kutumia helikopta, amesema Rashid Ahmed, Waziri wa Reli wa Pakistan.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, treni hiyo ya abiria ilikuwa ikielekea Rawalpindi ikitokea Karachi.

Taarifa za awali zinasema kuwa, chanzo cha ajali hiyo kilitokana na moto wa stovu wakati abiria mmoja alipokuwa katika jitihada za kuandaa kifunguakinywa.

Baadhi ya duru zinaripoti kutoka Pakistan kwamba, kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya vifo hivyo hasa kutokana na kuwa, hali ya baadhi ya majeruhi wa tukio hilo ni mbaya sana.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu