Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Iran yalikosoa Baraza la Usalama la UN kwa kuzembea mbele ya jinai za Israel

October 29, 2019

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameituhumu jamii ya kimataifa kwamba imefeli mbele ya sera za kujipanua za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi ya Palestina.

 

Es’haq Al-e Habib amekiambia kikao cha Baraza la Usalama kilichoitishwa kujadili maudhui ya Amani na Usalama Mashariki ya Kati na Kadhia ya Palestina kwamba, baraza hilo limepasisha karibu maazimio elfu 2,500, na 365 kati ya maazimio hayo yamehusu Palestina kwa njia moja au nyingine, lakini hakuna hata moja lililotekelezwa.

 

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ambaye pia alikuwa akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na vilevile Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kufanya ukatili na kukiuka sheria kwa himaya kamili ya baadhi ya nchi za Kimagharibi.

 

Es’haq Al-e Habib amesema kuwa uvamizi na uchokozi wa Israel dhidi ya majirani na kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, Lebanon na Syria ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na kuongeza kuwa, utawala huo unaendeleza sera za kujipanua kwa kujenga vitongoji zaidi vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Vilevile ameashiria silaha za mauaji ya halaiki za utawala huo ghasibu na kusema: Israel imekataa kutia saini mikataba yote inayohusiana na silaha za maangamizi ya umati na imetishia kuiangamiza nchi moja ya Mashariki ya Kati kwa kutumia silaha za nyuklia.

 

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa Israel inaendelea kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina na kwamba kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka uliopita wa 2018 peke yake utawala huo uliwaua Wapalestina 299 na kujeruhi wengine zaidi ya elfu 31.

Amesema wengi wa wahanga hao waliuawa wakifanya maandamano ya amani. Amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake na

kuzuia jinai na vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload