UN: Watu milioni 821 wanakabiliwa na njaa duniani


Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya milioni 821 katika pembe mbalimbali za dunia wanakabiliwa na baa la njaa; mwaka jana 2018 ukiwa mwaka wa tatu mfululizo kwa idadi hiyo kuongezeka kwa kiwango cha kutisha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) amesema katika hotuba yake huko Brussels mji mkuu wa Ubelgiji kwamba, idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni imeongezeka kutoka watu milioni 811 mwaka juzi 2017 hadi milioni 821 mwaka jana.

Ameeleza bayana kuwa mamilioni ya watu katika maeneo mbalimbali ya dunia wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na kukabiliwa na njaa.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaotaabika kwa janga la njaa katika maeneo tofauti ya dunia, kiwango ambacho kimeongezeka kutokana na mizozo ya kivita na mabadiliko ya tabianchi.

UN: Kiwango cha njaa duniani kimeongezeka kutokana na mizozo ya kivita na mabadiliko ya tabianchi

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP amefafanua kuwa, "Ni muhali kufikia dira ya Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ya kutokomeza baa la njaa duniani kikamilifu kufikia mwaka 2030."

Huku akikosoa namna vyombo vya habari vinavyochangamkia kadhia ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya (Brexit) na uongozi wa Rais Donald Trump wa Marekani na kupuuza kadhia muhimu ya njaa, afisa huyo wa ngazi za juu wa Mpango wa Chakula Duniani amebainisha kuwa, "hatuwezi kuwa na amani, usalama na uthabiti bila kuwa na usalama wa chakula."

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu