Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Iran yaitaka Uingereza kuachilia meli yake mara moja

July 13, 2019

Iran imeitaka Uingereza kuiachilia meli ya mafuta ya jamhuri hiyo ya Kiislamu ambayo jeshi la wanamaji la Uingereza waliizuia wiki kwa madai ya kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa kupeleka mafuta nchini Syria. 

Msemaji wa wizara ya nje ya Iran, Abbas Mousavi, ameliambia shirika la habari la nchi hiyo, IRNA, kuwa kitendo cha jeshi la Uingereza kilikuwa cha hatari na kitakuwa na athari zake kwa sababu hakuna sababu za kisheria za kuizuia meli hiyo.

 

Ameishtumu Uingereza kwa kuzuia meli hiyo chini ya shinikizo la Marekani, akisema hatua hiyo ilichukuliwa kinyume cha sheria na huenda ikaongeza taharuki katika Ghuba ya Uajemi.Iran imeonya kuchukuwa hatua sawa na hiyo iwapo meli hiyo haitaachiliwa.

 

 

 Uingereza ilisema kuwa meli tatu za Iran zilijaribu kuizuia meli inayomilikiwa na Uingereza iliyokuwa ikipita katika mlango bahari wa Hormuz, njia kuu ya usambazaji wa mafuta yanayotoka Ghuba kwenda katika maeneo mengine duniani lakini ikaondoa meli hizo baada ya kukabiliwa na meli ya kivita ya jeshi la wanamaji la Uingereza.

 

Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif, amekanusha madai hayo, akisema si mara ya kwanza kwa Uingereza kutumia mbinu kama hizo kuficha uovu wake.

 

Uingereza inadai kuwa meli hiyo ilikuwa ikipeleka mafuta nchini Syria iliyo chini ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya  lakini Iran imekanusha madai hayo na kusema kwamba haiko katika uanachama wa Umoja wa Ulaya na pia haihusiki na vikwazo vyovyote vya mafuta vya Umoja wa Ulaya.

 

www,nzunguko.com

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload