Takht-Ravanchi: Marekani inalisaidia genge la kigaidi la MKO kufanya jinai nchini Iran


Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Marekani inalisaidia kwa hali na mali genge la kigaidi la MKO lenye historia chafu ya kutenda jinai dhidi ya wananchi na maafisa wa Iran.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Majid Takht-Ravanchi akisema hayo jana jioni katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokuwa kinajadili suala la ugaidi na jinai za kitaasisi na kusema kuwa, Iran ni muhanga wa ugaidi na uhalifu huo wa kitaasisi.

Ameongeza kuwa, genge la kigaidi la MKO linaloungwa mkono na baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati na za Ulaya, linashirikiana kwa karibu na mashirika ya kijasusi ya Marekani kwa ajili ya kufanya uharibifu ndani ya Iran.

Amesema, kama ambavyo Iran iko mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi na uhalifu wa kitaasisi, yenyewe ni muhanga wa vitendo hivyo vya kigaidi kiasi kwamba hadi hivi sasa wananchi 17,161 wa Iran akiwemo rais wa nchi, waziri mkuu, mkuu wa vyombo vya mahakama na mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran pamoja na wabunge 27 na wanasayansi na wataalamu wakubwa wanne wa masuala ya nyuklia wa Iran wameshauawa kutokana na vitendo hivyo vya kigaidi vinavyoungwa mkono na madola ya Magharibi, baadhi ya nchi za eneo hilo na nchi za Ulaya.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa vile vile amesema, licha ya kwamba genge la MKO lilikuwemo kwenye orodha ya magenge ya kigaidi, lakini Marekani imelitoa kwenye orodha hiyo na kuwapa hifadhi magaidi hao nchini Marekani na inashirikiana nayo kwa karibu sana kujaribu kufanya uharibifu ndani ya Iran.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu