Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Baraza la Kijeshi Sudan: Tuko tayari kukabidhi muswada wa makubaliano na wapinzani

July 10, 2019

Baraza la Kijeshi la Sudan limesema kuwa, liko tayari kukabidhi muswada wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya baraza hilo na makundi mbalimbali ya wapinzani.

 

 

Kauli hiyo ilitolewa jana na kuongeza kuwa hati hiyo ya maelewano itakabidhiwa kwa makundi husika leo Jumatano ili yaweze kupitia kabla ya kutiwa saini na kuwa maafikiano rasmi.

 

Duru za kuaminika za Sudan zilikuwa zimesema kuwa, makubaliano baina ya Baraza la Kijeshi la Sudan na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko kuhusiana na kugawana madaraka ya serikali ya mpito, yatatiwa saini kesho Alhamisi.

 Habari nyingine zinasema kuwa, Sadiq al Mahdi, mkuu wa chama cha Umma cha Sudan amesema kuwa, kama wajumbe wa Baraza la Kijeshi la Sudan watakuwa tayari kuvua magwanda yao ya kijeshi na kuwa raia wa kawaida na kuingia katika siasa, basi chama chake cha umma kinawakaribisha kujiunga nacho.

 

Pande mbili za Baraza la Kijeshi la Sudan na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan, Alkhamisi ya wiki iliyopita zilifikia makubaliano maalumu ya kipindi cha mpito kwa upatanishi wa Umoja wa Afrika na Ethiopia. 

 

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka mitatu na miezi mitatu na baraza litakaloongoza nchi hiyo litakuwa na wajumbe watano wanajeshi na wajumbe watano raia. Uwenyekiti wa baraza hilo utakuwa ni wa kupokezana.

 

Katika kipindi hicho cha mpito kutaundwa serikali ya kiraia itakayosimamia masuala ya Sudan na kutaanzishwa Bunge jipya baada ya kuundwa serikali hiyo.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload