Uchumi wa nchi za Afrika kufikia kiwango cha dola trilioni 3.4


Uchumi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) unatazamiwa kuimarika na kufikia kiwango cha dola trilioni 3.4

Ndoto hii itatimia iwapo awamu ya utendaji ya Makubaliano ya Eneo Huria la Biashara Afrika (AfCFTA) iliyozinduliwa hapo jana na viongozi wa Afrika katika mji mkuu wa Niger, Niamey itatekelezwa ipasayo.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amepongeza uzinduzi huo na kusema, ni hatua ya kihistoria kwa bara la Afrika, hususan katika kutimiza ajenda ya maendeleo ya bara hilo ya mwaka 2063.

Eneo la Biashara Huria la Afrika lililozinduliwa mjini Kigali, Rwanda Machi 21 mwaka jana, linapendekeza kuwa na soko moja la bidhaa na huduma kwa bara hilo, huku kukiwa na uhuru wa maingiliano kwa wafanyabishara na wawekezaji, ili kutoa njia ya kuongeza kasi ya kuanzishwa kwa umoja wa forodha.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat

Nchi wanachama wa AU zimekubaliana kupunguza ushuru wa forodha miongoni mwao kwa asilimia kati ya 15-25, ili kuimarisha biashara na mabadilishano ya bidhaa.

Wachumi wanasema nchi 55 wanachama wa AU zimebaki nyuma na kushindwa kufikia kilele cha mafanikio katika uwanja wa uchumi na biashara kutokana na vizingiti vingi vya kibiashara.

Vizingiti hivyo vimekuwepo licha ya kuwepo na jumuiya kadhaa katika bara hilo, kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

www.mzunguko,com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu