Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Wananchi wa Yemen waonesha silaha zao mpya za kukabiliana na Saudia na wavamizi wenzake

July 8, 2019

Jeshi la Yemen na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo zimeonesha silaha zao mpya za kukabiliana na wavamizi wa nchi yao, Saudi Arabia, Imarati na wavamizi wengine. Sherehe hizo zimehudhuriwa na Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, Mahdi al Mashat.

 

Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo na kusema kuwa, sherehe hizo zilizofanyika jana, zimeonesha sehemu ndogo tu ya silaha mpya za ndroni (ndege zisizo na rubani) na kombora jipya la "Quds 1." Ndege zisizo na rubani zilizowekwa kwenye maonesha hayo ni pamoja na "Samad 1," "Samad 3" na "Qasif K2" zilizotengenezwa na wasomi na wataalamu wenyewe wa Yemen.

 

Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Yemen, Muhammad Nasir al Atifi, wataalamu wa kijeshi wa nchi hiyo wamepiga hatua kubwa za kiutalamu katika kutengeneza silaha za kijeshi ndani ya Yemen.

 

Moja ya silaha mpya zilizooneshwa hadharani na Jeshi la Yemen kwa ajili ya kukabiliana na wavamizi wa nchi yao wakiongozwa na Saudia.

 

Kabla ya hapo pia, jeshi la Yemen lilikuwa limeonesha hadharani makombora yake ya "Badr F" na "Badr 1 P."

 

Nguvu za kijeshi za kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen na jeshi la nchi hiyo zinazidi kuongezeka siku baada ya siku licha ya wavamizi wakiongozwa na Saudi Arabia, kuizingira kila upande nchi hiyo maskini ya Kiarabu, kutokea angani, baharini na ardhini.

 

Mwezi Machi 2015, Saudia iliunda muungano wa nchi kadhaa za Kiarabu na kuivamia kila upande nchi ya Waislamu ya Yemen kwa madai ya kutaka kumrejesha madarakani Abdu Rabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu mwenyewe na kukimbilia Saudi Arabia.

 

Wavamizi wa Yemen walitekwa na tamaa ya kumaliza vita vya nchi hiyo muda mchache tu, lakini hivi sasa mwaka wa tano umeshaingia, wavamizi hao wamefeli katika kila kitu huku wananchi wa Yemen wakizidi kuwa imara.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload