Wahamiaji 151 Waafrika waokolewa Morocco kwenye Bahari ya Mediterania


Jeshi la majini la Morocco limetangaza kuwa limewaokoa wahamiaji haramu 151 kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika wakiwa katika bahari ya Mediterania walipokuwa wakijaribu kuingia barani Ulaya.

Jeshi hilo limesema, vikosi vya jeshi la majini vilivyokuwa vikipiga doria katika bahari ya Mediterania usiku wa Jumamosi na alfajiri ya Jumapili, vilisaidia mashua 16 zilizokuwa zimekumbwa na matatizo katika Lango Bahari la Gibraltar na kuwaokoa wahamiaji 151.

Wahamiaji hao wamepelekwa salama kwenye bandari ya mji wa Tangier kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Morocco, jumla ya wahamiaji 88,761 walizuiwa kuondoka Morocco mwaka jana.

Aidha serikali ya Morocco imesema mwaka jana ilisambaratisha mitandao 229 ya magenge yanayohusika na usafirishaji haramu wa binadamu.

Umoja wa Ulaya umeipatia Morocco Euro milioni 30 kati ya 140 ilizoahidi Oktoba mwaka jana ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na wahamiaji haramu kutoka nchi za Afrika ambao wanatumia pwani ya nchi hiyo kuelekea Ulaya,

Nusu ya wahamiaji haramu 111,558 walioingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea mwaka 2018 walipitia njia ya magharibi ya pwani ya Peninsula ya Iiberia ambayo inatenganisha Ulaya na Afrika Kaskazini.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, wahamiaji 2,217 walipoteza maisha wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterranea kuelekea Ulaya ambapo miongoni mwao 744 walikuwa ni watoto.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu