Mtu mmoja auawa katika maandamano ya Wasudan eneo la Darfur


Mtu mmoja amepoteza maisha hii leo kutoka majeraha ya risasi aliyofyatuliwa hapo jana katika maandamano ya wananchi wa Sudan, ya kulishinikiza Baraza la Mpito la Kijeshi likabidhi madaraka kwa raia.

Jumuiya ya Madaktari Sudan imeripoti kuwa, kijana huyo kwa jina Saad Mohammed Ahmed aliyekuwa na umri wa miaka 18 ameaga dunia hii leo, kutokana na majeraha aliyoyapata jana Jumamosi, baada ya kupigwa risasi katika ghasia zilizoibuka kati ya maafisa usalama na waandamanaji katika eneo la Nyala mkoani Darfur.

Meja Jenerali Hashim Mahmoud, Gavana wa mkoa wa Dafur Kusini amesema takriban watu elfu tano walifanya maandamano jana Jumamosi, wakielekea katika kambi ya jeshi ya Nyala mkoani hapo, na ndipo maafisa usalama wakalazimika kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.

Baraza la Mpito la Kijeshi linalotawala nchini Sudan limekataa pendekezo la muundo wa Baraza la Utawala litakalokuwa na wanajeshi watatu na raia saba kwa ajili ya kuongoza kipindi cha mpito

Wakuu wa Baraza la Mpito wa Kijeshi la Sudan katika kikao na waandishi wa habari mjini Khartoum

Baraza hilo liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.

Wakati huohuo, duru za habari zimearifu kuwa, wananchi wa Sudan wanakabiliwa na uhaba wa fueli na mfumko wa bei za bidhaa,

wakati huu ambapo wanajitayarisha kuanza ibada ya funga ya mwezi Mtufuku wa Ramadhani. Maandamano ya kumng'oa madarakani al-Bashir yalichochewa kwa kupanda bei ya bidhaa muhimu kama mkate na mgogoro wa mafuta.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu