Baraza la Kijeshi Sudan lakataa pendekezo la muundo wa Baraza la Utawala wa Mpito


Baraza la Kijeshi linalotawala nchini Sudan limekataa pendekezo la muundo wa Baraza la Utawala litakalokuwa na wanajeshi watatu na raia saba kwa ajili ya kuongoza kipindi cha mpito.

Salah Abdel-Khaliq, mjumbe wa Baraza la Kijeshi la Sudan ametangaza leo kuwa, baraza hilo limekataa pendekezo la kuweko idadi kubwa ya raia katika baraza la watu 10 la kuendesha serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Salah Adel-Khaliq imeeleza kuwa, Baraza la Kijeshi la Sudan linataka kuweko idadi sawa katika baraza hilo la kuendesha serikali ya mpito yaani wanajeshi watano na raia watano.

Kamati ya upatanishi nchini Sudan ilikuwa imependekeza kuundwa kamati ya watu 10 ya mpito itakayojumuisha raia saba na wanajeshi watatu chini ya uenyekiti wa Baraza la Kijeshi la nchi hiyo.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

Licha ya kwamba jeshi la Sudan liliahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia baada ya maandamano ya kumng'oa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir, lakini hadi sasa limeshindwa kutekeleza ahadi yake hiyo.

Baraza la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.

Baraza hilo lina wajumbe 9 wakiwemo wanajeshi sita, polisi wawili na afisa mmoja wa masuala ya kijasusi na usalama wa taifa.

www,mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu