Waliouawa katika hujuma za kigaidi Sri Lanka wakaribia 300


Idadi ya watu waliopoteza maisha katika hujuma za kigaidi nchini Sri Lanka inakaribia 300 huku wakuu wa usalama nchini humo wakitangaza kuwa wamewakamata washukiwa 24.

Kwa mujibu wa taarifa, hadi sasa watu 290 wamethibitishwa kupoteza maisha katika hujuma hizo ambazo zililenga makanisha na mahoteli ya kifahari huku idadi hiyo ikitazamiwa kuongezeka

Mashambulizi manane ya mabomu yaliyoratibiwa kwa pamoja yaliwalenga waumini wa Kikristo waliokuwa wakishiriki katika ibada za Pasaka na wageni wa kimataifa katika hoteli za kifahari nchini humo.

Msemaji wa polisi nchini Sri Lanka amesema hadi sasa watu 500 wamethibitishwa kujeruhiwa katika hujuma hizo za kigaidi ambazo zililenga makanisa matatu, hoteli nne za kifahari na nyumba.

Wakati huo huo, bomu la kujitengenezea limegunduliwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege mjini Colombo na tayari limeshateguliwa.

Hadi sasa hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na hujuma hizo za kigaidi huku polisi wakisema wamewakamata washukiwa 24.

Wapelelezi wanasema wanachunguza iwapo waliotekeleza hujuma hizo za kigaidi wana uhusiano wowote na mitandao ya kimataifa.

Raia wa kigeni waliouawa katika hujuma hizo ni kutoka India, Uingereza, Marekani, Uturuki, Ureno na Japan.

Mkuu wa Polisi Sri Lanka Pujuth Jayasundara amesema walipokea taarifa siku 10 zilizopita kuwa magaidi walikuwa wanalenga kutekeleza hujuma dhidi ya makanisha na ubalozi wa India mjini Colombo. Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe amesema watachunguza ni kwa nini hatua za kutosha hazikuchukuliwa kuzuia hujuma hizo za kigaidi.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu